Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, amefanya kikao muhimu na Viongozi wa Jumuiya ya Wanasayansi wa Kilimo Mazao (CROSAT) katika ofisi yake jijini Dodoma, ambapo ameahidi kuendeleza ushirikiano kati ya Serikali kupitia Wizara ya Kilimo na Jumuiya hiyo ili kuongeza tija na maendeleo kwenye sekta ya kilimo nchini.
Katika kikao hicho, Waziri Bashe ameeleza kuwa Serikali inatambua mchango mkubwa wa wataalamu na wanasayansi wa kilimo, na kwamba ushirikiano wa karibu na CROSAT ni nyenzo muhimu katika kufanikisha mipango ya kuendeleza kilimo chenye tija, chenye kutumia sayansi, teknolojia na ubunifu.
“Niwahakikishie kuwa Wizara ya Kilimo ipo tayari kuendelea kushirikiana nanyi kwa karibu katika kuhakikisha tunaleta mageuzi ya kweli katika sekta ya kilimo, hususan katika upande wa utafiti wa kisayansi na matumizi ya teknolojia katika uzalishaji,” alisema Bashe.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa CROSAT, Ndugu Patrick Ngwediagi, ametoa pongezi kwa Waziri na Wizara ya Kilimo kwa namna ambavyo wamekuwa bega kwa bega na Jumuiya hiyo katika kusimamia ajenda ya maendeleo ya kilimo. Alieleza kuwa ushirikiano huo umekuwa chachu ya mafanikio katika mipango na miradi mbalimbali ya utafiti na mafunzo kwa wataalamu wa kilimo.
“Tunashukuru sana Wizara kwa kutambua nafasi ya CROSAT katika sekta ya kilimo. Ushirikiano huu umeonesha matokeo chanya, na tunaamini kuwa kwa kuimarisha zaidi mahusiano haya, sekta ya kilimo nchini itaendelea kupata mafanikio makubwa,” alisema Ngwediagi.
CROSAT ni Jumuiya ya kitaaluma iliyoundwa kwa lengo la kuwaunganisha Wanasayansi wa Kilimo Mazao nchini, na kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya sekta hiyo kwa njia ya tafiti, mafunzo na ushauri wa kitaalamu. Jumuiya hiyo inajumuisha wataalamu kutoka taasisi mbalimbali za elimu, utafiti, pamoja na sekta binafsi.
Kupitia ushirikiano huu unaoendelea kuimarishwa, inatarajiwa kuwa Tanzania itaendelea kuwa na kilimo cha kisasa chenye tija, chenye kuchochewa na sayansi na ubunifu wa ndani.