Katika jitihada za kuimarisha ushirikiano baina ya taasisi za kifedha na mihimili ya Serikali, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Biashara Tanzania (TCB), Adam Mihayo amemtembelea na kuzungumza na Spika wa Bunge la Tanzania Dkt. Tulia Ackson.
Mihayo ameambatana na Mkurugenzi wa Biashara za Wateja Wadogo na wa Kati wa benki hiyo Lilian Mtali, katika ziara hiyo ambayo inafungua ukurasa mpya wa ushirikiano baina ya Benki ya TCB na Bunge la Tanzania katika kuwainua wajasiriamali wadogo na wa kati nchini.
Mazungumzo baina ya Mihayo na Dkt. Tulia yamejikita katika masuala nyeti yanayohusu majimbo mbalimbali katika jitihada za kuendelea kuwainua wajasiriamali wadogo na wa kati ambao ni muhimu katika ukuaji uchumi na uzalishaji wa ajira mpya.
Masuala hayo ni mpango wa utoaji wa mikopo yenye riba nafuu kwa wajasiriamali utakaosaidia kukuza na kuchochea mazingira ya biashara kwa wajasiriamali pamoja na biashara zao.
“Lengo letu sio kutoa jibu moja kwa nchi nzima. Huwezi kuwa na suluhisho moja kwa watu wote, ndiyo maana ni muhimu kuwasikiliza wadau wengi iwezekanavyo. Njia hii itatusaidia kutoa majibu yatakayokidhi mahitaji ya wajasiriamali kulingana maeneo wanayoishi hata wale walioko vijijini,” amesema Mihayo.
Kwa upande wake wake Dkt. Tulia Ackson amebainisha umuhimu wa ushirikiano huo na kusisitiza wajibu wa Bunge katika kutunga sera zinazowezesha maendeleo ya wajasiriamali na kuhakikisha kwamba biashara zao zinapata rasilimali zinazohitajika ili kukua.
“Maendeleo ya wajasiriamali ni muhimu kwa ukuaji uchumi wa taifa letu, kupitia ushirikiano huu na Benki ya TCB, tunaweza kutengeneza mazingira yatakayowezesha ukuaji wa biashara”, amesema.
Kikao hicho kimehitimishwa kwa azimio la ushirikiano wa pamoja na kuendelea kubuni nyanja mbalimbali za ushirikiano lengo likiwa kuinua sekta ya wajasiriamali.