Tarehe 5 Novemba 2024, Benki ya Equity Tanzania ilisaini mkataba na Taasisi ya ADC Tanzania, washauri wabobezi wa biashara, kuashiria kuanza kwa utekelezaji wa mradi maalum wa kuwawezesha wanawake kiuchumi kupitia programu inayoitwa Jifunze Utoke Program.
Mradi huu unafanyika kwa ushirikiano na Taasisi ya Maendeleo ya Kimataifa ya African Guarantee Fund/AFAWA, ukilenga kuwajengea wanawake uwezo katika biashara zao ili waweze kufikia vigezo vya kupata huduma mbalimbali za kifedha, ikiwemo mikopo inayotolewa na Benki ya Equity, ili kuboresha maisha yao kijamii na kiuchumi.
Meneja Mkuu wa Biashara wa Benki ya Equity Tanzania Leah Ayoub, amesema mradi huo ni sehemu ya mpango mkakati wa Benki ya Equity wa kuongeza wigo wa huduma kwa wateja wadogo na wa kati (MSMEs), kwa lengo la kufikia 65% ya mikopo yote ifikapo mwaka 2030.
“Tukiwa na dhamira ya kuwawezesha wanawake katika biashara, ushirikiano huu ni hatua muhimu ya kuboresha upatikanaji wa huduma za kifedha kwa wanawake wajasiriamali na kuwawezesha kufikia ukuaji wa kiuchumi endelevu,” amesema Leah.
Naye, Afisa Biashara kutoka ADC, Laura Vedasto ameeleza kuwa ni muhimu kwa wanawake wanaotarajiwa kusaidiwa kujifunza kuratibu namna nzuri ya kutumia pesa wanazozipata ili ziwasaidie kukuza biashara zao.
“Ukisema ‘Jifunze Utoke, inamaanisha kwamba licha ya ukweli kwamba tunataka kuwafunza na kuwasaidia hawa wanawake, lakini ni lazima kwanza wajifunze, wajue ni jinsi gani wanaweza kutumia vyema mitaji yao, hata kama hizi hela wakipewa wanatakiwa kuzitumia vipi ili kuweza kupata biashara ambayo inakua, na wakati huohuo iweze kuwafaidisha wote”, ameeleza Laura.
Mradi huu unalenga kuwawezesha zaidi wanawake nchini Tanzania kwa kuwapatia mafunzo ya elimu ya fedha, mikopo nafuu, na ushauri maalum wa biashara.
Kwa hatua hii, Benki ya Equity Tanzania inaendelea kujitolea kuimarisha uimara wa kiuchumi na ujumuishi wa kijamii nchini. Matangazo zaidi ya hatua za mradi huu yatafuata kadri mradi unavyosonga mbele.