Serikali imeendelea kuchukua hatua kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma bora za mawasiliano nchini, ambapo kupitia mradi wa minara 758, wananchi takribani milioni 8.5 katika mikoa 26 ya Tanzania Bara watanufaika kwa gharama ya shilingi bilioni 126.
Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), Mhandisi Peter Mwasalyanda, ameeleza hayo wakati wa mkutano na waandishi wa habari Machi 27, 2025, katika Ofisi za Idara ya Habari – MAELEZO, jijini Dodoma, akielezea mafanikio na mwelekeo wa mfuko huo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita.
Mwasalyanda amesema mradi huo wa kimkakati unalenga kufikisha mawasiliano kwa vijiji 1,007, kata 713, na wilaya 127. Mpaka sasa, tayari minara 430 kati ya 758 imekamilika.
“Pamoja na mradi huu, tumeboresha minara 304 kwa kuongeza nguvu kutoka 2G hadi 3G, kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni 5,” amesema.
Ameongeza kuwa dhamira ya serikali ni kuhakikisha wananchi wanapata mawasiliano ya uhakika, kwani maendeleo ya kiuchumi yanategemea mtandao madhubuti.
Katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita, serikali pia imewapatia mafunzo ya TEHAMA walimu 1,585 ili kuwajengea uwezo wa kutatua changamoto za vifaa vya kidigitali.
Jumla ya walimu 3,798 wamepata mafunzo hayo kutoka shule 1,791, ambapo kwa upande wa Zanzibar, walimu 326 wamenufaika huku Tanzania Bara, walimu 3,180 wakinufaika.
Mhandisi Mwasalyanda amesisitiza kuwa jitihada hizi za kuboresha mawasiliano zinachochea maendeleo kwa kuongeza fursa za biashara, elimu, na huduma za kidijiti kwa wananchi wote.