Mwanafunzi wa Shule ya Msingi Jamhuri wilayani Mbarali wamenufaika na mradi wa maji uliotekelezwa na Bodi ya Maji Bonde la Rufiji kupitia mradi wa NBS Usangu, unaofadhiliwa na Serikali ya Japan kwa kushirikiana na Benki ya Dunia.
Mradi huo, uliozinduliwa na Mwakilishi wa Balozi wa Japan nchini Tanzania, umewezesha kuchimbwa kwa kisima kirefu na kusambaza maji shuleni pamoja na kwa wananchi wa maeneo jirani.

Inaelezwa kabla ya utekelezaji wake, wanafunzi walilazimika kutembea zaidi ya kilometa tatu kufuata maji, hali iliyokuwa ikiathiri masomo na usalama wao.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Mkurugenzi wa Bodi, Mhandisi David Munkyala, alisema lengo la mradi ni kuboresha upatikanaji wa maji huku ukizingatia uhifadhi wa mazingira.
Kwa upande wake, Mratibu wa Mradi, David Muginya, alisisitiza umuhimu wa ushirikishwaji wa jamii ili kuhakikisha mradi unakuwa endelevu na wenye manufaa ya muda mrefu.
