Latest Posts

BODI YA WAKURUGENZI YA CRB YARIDHISHWA NA UJENZI WA UWANJA WA NDEGE SHINYANGA NA RELI YA KISASA YA SGR

Bodi ya Wakurugenzi pamoja na Menejimenti ya Bodi za Usajili wa Makandarasi (CRB) wamekagua na kuridhishwa na ujenzi wa Mradi wa Ukarabati na Uboreshaji wa Uwanja wa Ndege wa Shinyanga pamoja na Mradi wa kusanifu na kujenga njia ya reli ya kisasa na stesheni ya Standard Gauge (SGR) kipande cha tano kutoka Mwanza hadi Isaka, iliyoko eneo la Malampaka.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa CRB, Mhandisi Joseph Nyamhanga, ameeleza hayo wakati wa ukaguzi wa ujenzi wa Mradi wa Ukarabati na Uboreshaji wa Uwanja wa Ndege unaotekelezwa na Mkandarasi China Henan International Cooperation Group (CHICO) pamoja na Mradi wa SGR unaotekelezwa kwa ubia na Makandarasi China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC) na China Railway Construction Corporation (CRCC) mkoani Shinyanga.

“Tumeona na kuridhishwa na kazi nzuri inayofanywa na Mkandarasi CHICO, wakizingatia ubora wa kazi na kufuata sheria za Usajili wa Makandarasi. Tumaini letu ni kwamba mradi huu utakamilika kwa wakati ili uanze kuleta manufaa ya kijamii na kiuchumi,” amesema Mhandisi Nyamhanga.

Pamoja na hayo amempongeza Mkandarasi China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC), na China Railway Construction Corporation (CRCC) kwa usimamizi mzuri wa utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa kusanifu na kujenga  stesheni na njia ya reli ya kisasa (SGR), kipande cha Isaka – Mwanza chenye urefu wa kilometa 3

“Tunaona mradi huu unaendelea vizuri na utakapokamilika hadi Mwanza utaleta manufaa makubwa kwa nchi yetu, kama tulivyoanza kuona kwa kipande kilichokamilika kutoka Dar es Salaam, Morogoro hadi Dodoma,” ameongeza Mhandisi Nyamhanga.

Hata hivyo, Mhandisi Nyamhanga amepongeza hatua iliyofanywa na Makandarasi wa miradi hiyo kwa ushirikishwaji mzuri wa makandarasi wa ndani, akisisitiza umuhimu wa kuwajengea uwezo katika kutekeleza miradi mikubwa nchini.

“Moja ya majukumu ya Bodi ni kuwaendeleza makandarasi wa ndani kwa kuhakikisha wanashirikishwa katika miradi mikubwa inayoendelea kutekelezwa nchini,” alisema Mhandisi Nyamhanga.

Aidha, ametoa wito kwa makandarasi wote nchini kufanya kazi kwa kuzingatia ubora na thamani ya mikataba ya miradi ya ujenzi.

Naye, Naseer, Mhandisi Mkazi Mshauri wa mradi kutoka SMEC Engineering International, amesema kuwa hadi sasa wameshakamilisha ujenzi wa ukarabati na uboreshaji wa uwanja wa ndege wa Shinyanga kwa asilimia 72, ikiwa ni pamoja na njia ya kurukia ndege yenye urefu wa kilomita 2.2.

“Mpaka sasa tumeshakamilisha vipengele muhimu, ikiwa ni pamoja na njia ya kurukia ndege, jengo la abiria, wigo, na mfumo wa kuongoza ndege,” amesema Mhandisi Naseer.

Mkandarasi CHICO anayetekeleza mradi huo ameahidi kukamilisha ujenzi kwa wakati kulingana na mkataba.

Sambamba na hayo, Mhandisi Samweli Mwambungu, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Shinyanga, amesema kuwa mradi wa ujenzi wa upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Shinyanga unahusisha ujenzi wa kiwanja cha ndege na jengo la abiria.

“Hadi kufikia sasa, mkandarasi amefanikisha ujenzi wa barabara ya kurukia ndege na kazi kubwa imebakia katika umaliziaji wa jengo la abiria. Kufikia mwezi Novemba, watahakikisha ujenzi huo umekamilika kwa asilimia 100 ili uanze kutoa huduma kwa wananchi,” amesema Mhandisi Mwambungu.

Kwa upande wake, Justine Mazinge, Mhandisi wa Viwango na Ubora katika mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa kipande cha Mwanza – Isaka, amesema maendeleo ya mradi hadi sasa ni asilimia 60.5, ambapo ujenzi mkubwa wa matuta na miundombinu ya madaraja umekamilika huku ujenzi wa reli na miundombinu ya umeme ukiendelea.

Aidha, mkandarasi CCECC anayetekeleza mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa SGR kipande cha tano kutoka Mwanza hadi Isaka ameahidi kukamilisha mradi huo kwa wakati, akizingatia ubora wa kazi kwa mujibu wa mkataba.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!