Baada ya kukwama tarehe 23/09/2024 kwa hukumu ya dhamana ya aliyekuwa Meya wa Manispaa ya Kinondoni na baadaye Ubungo Boniface Jacob maarufu kama ‘Boni Yai’ ambaye ameshtakiwa kwa makosa ya mtandao leo, tarehe 26/09/2024 chini ya Hakimu mkazi Mkuu Franco Kiswaga wa Mahakama ya Hakimu mkazi Kisutu, Dar es Salaam, Meya huyo wa zamani ataendelea kusota magereza hadi juma lijalo baada ya hukumu ya kesi ndogo ndani ya kesi ya msingi iliyotarajiwa kusomwa Mahakamani hapo ‘kushindikana’
Awali kesi hiyo ilitarajiwa kuanza saa tano kamili asubuhi ya leo, lakini licha ya Boniface Jacob ambaye pia ni mfanyabiashara na kada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kufikishwa Mahakamani hapo majira ya saa 04 asubuhi lakini alipandishwa kizimbani saa 09:30 alasiri
Kabla ya Mahakama kuanza kusoma hukumu yake, upande wa waleta maombi uliiomba Mahakama hiyo iridhie kuondoa shauri la kwanza kati ya mawili yaliyowasilishwa yaliyotarajiwa kutolewa maamuzi kwa kile kilichodaiwa kuwa shauri hilo lililetwa kimakosa Mahakamani hapo
Ikumbukwe kuwa Mahakama hiyo ilitarajiwa kutoa maamuzi madogo mawili, la kwanza likiwa ni ombi la Jamhuri kumuamuru mshtakiwa Boniface Jacob atoe nywila (password) za simu zake mbili (2) wanazoshikilia na zile za akaunti yake ya mtandao wa X (zamani twitter) ili ziweze kuingiliwa ikiwa ni sehemu ya kukamilisha upelelezi
Wakati ombi la pili la Jamhuri lililotarajiwa kutolewa maamuzi madogo ni lile la kuiomba Mahakama kuzuia dhamana ya Boniface Jacob, hiyo ikitokana na kiapo cha RCO wa mkoa wa Kipolisi Kinondoni kilichowasilishwa Mahakamani hapo kikieleza kuwa usalama wa Meya huyo wa zamani uko endapo atakuwa ‘uraiani’, hivyo Mahakama isimpatie dhamana ili kulinda usalama wake
Baada ya upande wa Jamhuri kuwasilisha ombi la kuondolewa kwa shauri la kwanza kati ya mawili (2) yaliyotarajiwa kutolewa maamuzi, upande wa utetezi ukiongozwa na Wakili wa kujitegemea Peter Kibatala ulipinga vikali hoja hiyo, na kuiomba Mahakama hiyo kuendelea na ratiba yake ya kusoma hukumu hiyo
Hata hivyo baada ya kushuhudiwa mivutano ya kisheria kutoka kwa Mawakili wa pande zote mbili, na baada ya Mahakama kupitia vifungu kadhaa vya sheria na kurejea baadhi ya kesi za aina hiyo hatimaye Hakimu mkazi Mkuu Franco Kiswaga wa Mahakama ya Hakimu mkazi Kisutu alikubaliana na hoja zilizowasilishwa na Jamhuri na kuondoa shauri hilo
Miongoni mwa sababu zilizowasilishwa na Jamhuri zilizopelekea kuomba kuondoa shauri hilo ni pamoja na kwamba wakati linawasilishwa na kusikilizwa Mahakamani hapo kulikuwa na kasoro kadhaa ambazo kwenye mazingira ya kawaida endapo ingeendelea kubaki kwenye kumbukumbu za Mahakama ingetumika kama mifano siku za usoni na kupotosha baadhi ya mashauri
Hata hivyo baada ya Mahakama kuridhia ombi hilo, upande wa Jamhuri ulikuja na maombi mengine ya kuongeza kiapo cha ziada kwenye shauri lililobaki ambalo kimsingi ni shauri la pili (2) lile linalohusu kuiomba Mahakama kutompatia dhamana Boniface Jacob kutokana na kulinda usalama wake, na hapo ndipo walipowasilisha kiapo cha ziada cha RCO wa mkoa wa Kipolisi Kinondoni
Jambo hilo pia liliibua mjadala mpana na majibizano miongoni mwa Mawakili wa pande zote mbili, kwa kuwa upande wa utetezi ukiongozwa na Wakili Kibatala ulidai kuwa kiapo hicho hakikubaliki kwa kuwa kimeletwa Mahakamani hapo kinyume cha sheria hivyo kinapaswa kutupiliwa mbali
Wakili Kibatala na jopo lake waliwasilisha mapingamizi kadhaa ya kisheria na kurejea baadhi ya kesi ili kuishawishi Mahakama kutupilia mbali maombi hayo, badala yake ijikite kubaki kwenye ratiba ya msingi ya kusoma hukumu ndogo iliyotarajiwa, mapingamizi ambayo pia yalijibiwa kisheria na waleta maombi wakiongozwa na Wakili wa serikali mwandamizi Job Mrema
Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, Hakimu mkazi Mkuu Franco Kiswaga wa Mahakama ya Hakimu mkazi Kisutu, Dar es Salaam akaahidi kutoa maamuzi madogo ya mashauri hayo Jumatatu ya Oktoba 01.2024 majira ya saa 03:00 asubuhi
Hoja zinazotarajiwa kutolewa maamuzi na Mahakama ni pamoja na kwamba kama kiapo cha RCO wa mkoa wa Kipolisi Kinondoni kilichowasilishwa Mahakamani hapo kimewasilishwa ndani ya muda stahiki, na kama kimewasilishwa kwa mujibu wa sheria au la
Upande wa Jamhuri/serikali katika kesi hiyo unawakilishwa na Mawakili wanne (4) wakiongozwa na Wakili wa serikali mwandamizi Job Mrema huku upande wa utetezi/upande wa Jacob ukiwakilishwa na Mawakili saba (7) wakiongozwa na Wakili wa kujitegemea Peter Kibatala
Hivyo basi, Boniface Jacob ataendelea kusalia mahabusu mpaka siku hiyo, hata hivyo upande wa utetezi uliiomba Mahakama kuishinikiza Jamhuri kumleta Mahakamani mtuhumiwa kwani Septemba 23.2024 walishindwa kumleta kwa kile walichodai kuwa uwepo wa ’tishio’ la kiusalama
Jamhuri imeahidi kutekeleza maagizo hayo ya Mahakama ingawa imetoa tahadhari kuwa haiwezi kubashiri hali ya mazingira ya siku za usoni, jambo ambalo limemlazimu Hakimu kusema kuwa endapo mtuhumiwa hataletwa Mahakamani itaendesha shauri hilo kwa njia ya mtandao (video conference) hivyo kuahidi kuwa haiwezi kukwama.