Latest Posts

BOT YAJITETEA, WACHUMI NA WANASIASA WAKINZANA KUHUSU HATIMA YA DHAHABU

Mjadala mkubwa kuhusu kuuzwa kwa sehemu ya dhahabu ya Tanzania umeendelea kupamba moto nchini, huku kukiwa na mivutano ya kimitazamo kati ya wasimamizi wa sera za kifedha, wanasiasa, na wachumi wabobezi.

Hii ni baada ya kuibuka kwa taarifa mitandaoni zikidai kuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ina mpango wa kuuza sehemu ya hifadhi ya dhahabu ili kufadhili miradi ya kimkakati ya serikali, hoja iliyozua hofu, maswali na mitazamo kinzani miongoni mwa wananchi, wachumi na wanasiasa.

“Watanzania mnajua kwamba kuna uamuzi mkubwa kama huu umefikiwa? Kila kitu kinauzwa kienyeji…hifadhi yetu inateketezwa…Hili sio jambo la kufanyika kimyakimya, huu ni uamuzi mkubwa, unaohitaji mjadala mkubwa”, aliandika Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Bara, John Heche kupitia mtandao wa Instagram kama mmoja kati ya Watanzania wengine walioeleza hisia zao kuhusu taarifa hiyo.

Hata hivyo, BoT imekanusha madai hayo ikisisitiza kuwa hakuna mpango wowote wa kutumia dhahabu kufadhili miradi ya serikali. Akizungumza Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Idara ya Masoko ya Fedha wa BoT, Emmanuel Akaro, amesema kinachotekelezwa ni uamuzi wa kitaalamu wa kusawazisha mizania ya hifadhi ya dhahabu baada ya thamani yake kuvuka kiwango kilichoidhinishwa na bodi ya benki hiyo.

Kwa mujibu wa Akaro, bodi ya BoT imeidhinisha kiwango cha juu cha hifadhi ya dhahabu kisichozidi dola za Marekani bilioni mbili, wakati thamani ya sasa imefikia dola bilioni 3.24, hali inayolazimu kuuza kiasi kilichozidi ili kurejesha uwiano unaokubalika katika hifadhi ya fedha za kigeni. Amefafanua kuwa fedha zitakazopatikana hazitaelekezwa kwenye miradi ya serikali bali zitawekezwa katika masoko ya fedha ya kimataifa kwa lengo la kuongeza mapato ya uwekezaji wa benki hiyo.

Naye Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba, amewataka wananchi kupuuza kauli zinazopotosha zinazodai kuwa nchi haina fedha na inalazimika kuuza dhahabu ili kuendesha miradi yake. Akizungumza bungeni Januari 30, 2026, Dkt. Mwigulu alisema BoT ni taasisi imara inayozingatia misingi ya sera za kifedha na kwamba maamuzi yake yanafanywa kwa uangalifu mkubwa.

Dkt. Mwigulu, ambaye ni mtaalamu wa uchumi na aliyewahi kuwa Waziri wa Fedha, ameongeza kuwa BoT hununua dhahabu kutoka kwa wachimbaji wadogo kama njia ya kukuza uchumi wao, na inapofikia kipindi ambacho bei ya dhahabu duniani imepanda, benki inaweza kuuza sehemu ya akiba ili kupata fedha za kununua dhahabu zaidi kutoka kwa wachimbaji hao, hususan wadogo, na hivyo kuendeleza mzunguko wa uzalishaji wa ndani.

Hata hivyo, baadhi ya viongozi wa upinzani na wachumi wameonya juu ya hatari za kuangalia dhahabu kama rasilimali ya biashara badala ya kinga ya taifa dhidi ya mishtuko ya kiuchumi duniani. Kiongozi mstaafu wa ACT Wazalendo ambaye pia ni mchumi, Zitto Kabwe ameweka bayana tofauti ya kisheria kati ya dhahabu ya Benki Kuu na dhahabu ya Serikali, akisisitiza kuwa dhahabu ya BoT haiwezi kuuzwa kufadhili miradi ya serikali.

“Kuna dhahabu ya Benki Kuu ambayo inawekwa kama inavyowekwa akiba ya fedha za kigeni. Vilevile kunaweza kuwa na dhahabu ya serikali. Dhahabu ya BoT haiwezi kuuzwa kwa ajili ya miradi ya Serikali, ni mali ya BoT. Kisheria haiwezekani…itakuwa kinyume na sheria ya Benki Kuu kifungu cha 51 na 52. Kama ilivyo kwa akiba ya fedha za kigeni, akiba ya dhahabu ya Benki Kuu haiwezi kufadhili miradi ya Serikali…Dhahabu ya Serikali inaweza kuuzwa, ni mali ya Ssrikali, BoT inakuwa ni mtunzaji tu kama vile serikali inavyoweka fedha kwenye akaunti yake Benki Kuu ambapo akiba ya fedha za kigeni sio fedha za serikali kama ilivyo akiba ya dhahabu ya BoT sio dhahabu ya serikali”, ameandika Zitto Kabwe kupitia mtandao wa X.

Katika ushauri wake, kiongozi huyo amependekeza Serikali kutumia fursa ya bei nzuri ya dhahabu duniani kuwekeza zaidi kwa wachimbaji wadogo na wa kati, kununua dhahabu kwa kutumia shilingi ya Tanzania, na kuitumia kulipa sehemu ya deni la taifa la fedha za kigeni, hatua ambayo ingeongeza wigo wa kifedha wa serikali bila kuhatarisha hifadhi ya kimkakati ya taifa.

Naye Mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA, Godbless Lema, amehoji mantiki ya kuuza dhahabu wakati huu ambapo dunia inakabiliwa na misukosuko ya kisiasa na kiuchumi. Amedai kuwa dhahabu si mali ya kufanyia biashara bali ni kinga dhidi ya kuporomoka kwa thamani ya sarafu nyingine.

“Kuuza kwasababu thamani imepanda ni sawa na kuuza bima/kinga kabla hatari haijatokea. ‘Central banks’ makini huongeza dhahabu inapopanda bei, si kuuza. Fedha zinazotokana na mauzo ya dhahabu kwenda masoko ya fedha ya kimataifa ni hatari. Masoko hayo yana currency risk, interest rate risk, na counterparty risk, wakati dhahabu haina issuer risk. Hivyo, central banks hazifukuzi yield, bali zinalinda uthabiti wa taifa”, ameandika Lema kupitia mtandao wa Instagram.

Mjadala huo umechukua sura ya kitaalamu zaidi baada ya mchumi mkongwe Profesa Anna Tibaijuka kueleza kuwa dhahabu ni mtaji wa taifa na uamuzi wa kuinunua kuanzia mwaka 2023 ulikuwa sahihi. Akizungumza na Crown TV, Profesa Tibaijuka amesema hoja si kuuza au kutouza dhahabu, bali ni namna Serikali inavyosimamia matokeo ya mauzo hayo. Ameonya kuwa dhahabu ikishauzwa haiwezi kurejeshwa kirahisi, hivyo fedha zake lazima zielekezwe kwenye miradi yenye tija ya muda mrefu kama reli ya SGR, badala ya miradi isiyoleta faida ya kiuchumi.

“Kuna miundominu mingine hapa haina tija yoyote. Tulijenga uwanja wa ndege kule Chato, sijui kama unatusaidia kitu chochote. Kwahiyo unakuta kwamba tunauza dhahabu kufanya nini? Mimi nafikiria kuna reli yetu SGR, sasa ile nayo inatakiwa ikamilishwe kwasababu SGR ikiishia pale Dodoma matokeo ya huo uwekezaji huwezi kusema umeyapata”, ameeleza.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!