Na Amani Hamisi Mjege.
Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeripoti kuimarika kwa upatikanaji wa fedha za kigeni katika robo ya tatu ya mwaka 2024.
Kulingana na taarifa iliyotolewa siku ya Alhamisi Oktoba 03, 2024 na Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba, akiba ya fedha za kigeni imeongezeka kutoka dola za Marekani milioni 5,345.5 mwezi Juni hadi dola milioni 5,413.6 mwishoni mwa Septemba 2024.
Ongezeko hili limetajwa kuchangiwa na mauzo ya mazao nje ya nchi, sekta ya utalii, na kupanda kwa bei ya dhahabu kwenye soko la dunia. Aidha, mwenendo wa mauzo ya bidhaa asilia kama korosho, tumbaku, kahawa, na pamba umeelezwa kuendelea kuchangia ongezeko la mapato ya fedha za kigeni.
“Upatikanaji wa fedha za kigeni unatarajiwa kuendelea kuimarika, kutokana na ongezeko la bei ya dhahabu kwenye soko la dunia, shughuli za utalii na mauzo ya bidhaa asilia kama korosho, tumbaku, kahawa na pamba,” ameeleza Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba.
Pamoja na hilo, BoT imeeleza kuwa imefanikiwa kudhibiti kasi ya kushuka kwa thamani ya shilingi ya Tanzania, ambapo kwa mwaka unaoishia Septemba 2024, thamani ya shilingi iliporomoka kwa asilimia 10.1, ikilinganishwa na asilimia 12.5 mwaka uliopita.
Kulingana na taarifa hiyo, akiba ya fedha za kigeni sasa inatosheleza uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje kwa zaidi ya miezi minne, hali inayodumisha usalama wa kiuchumi wa taifa.
“Vilevile, matakwa ya kisheria kuhusu kunukuu na kufanya malipo ya ndani kwa shilingi ya Tanzania yanatarajiwa kupunguza mahitaji ya fedha za kigeni nchini na kuongeza ufanisi wa sera ya fedha”, ameeleza Tutuba.