Latest Posts

BUNDA KUJENGA JENGO LA GHOROFA LA MILIONI 432 KUIMARISHA MAPATO YA HALMASHAURI

Halmashauri ya Mji wa Bunda imepanga kutumia shilingi milioni 432 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la kisasa la ghorofa kama sehemu ya mpango wa kuongeza vyanzo vya mapato kupitia vitega uchumi vitakavyoongeza shughuli za kibiashara katika mji huo.

Akizungumza mbele ya Baraza la Madiwani, Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Juma Haji Juma, alisema kuwa jengo hilo linalotarajiwa kujengwa litakuwa na matumizi mbalimbali ya kibiashara na ofisi, na litaongeza mapato ya ndani ya halmashauri sambamba na kuimarisha shughuli za uchumi kwa wananchi wa Bunda.

Kauli hiyo ilikuja kufuatia hoja ya Diwani wa Kata ya Guta ambaye alitaka kufahamu kama utekelezaji wa mradi huo utakwamisha miradi mingine ya maendeleo ambayo pia imepangwa kutekelezwa.

Mkurugenzi alisisitiza kuwa mradi huo hautakwamisha miradi mingine na kwamba halmashauri imejipanga kutekeleza miradi yote kwa wakati, ikiwa ni pamoja na kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani ili kuleta maendeleo ya haraka kwa wananchi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Bunda, Michael Kweka, alisema kuwa mradi huo unakwenda sambamba na dhamira ya kuifanya Bunda kuwa wilaya ya kiuchumi na kivutio cha wawekezaji, kutokana na nafasi yake kama lango kuu la kuingia Mkoa wa Mara.

Naye Katibu Tawala wa Wilaya ya Bunda, Salum Mtelela, aliitaka halmashauri hiyo kuendelea kuongeza kasi ya ukusanyaji wa mapato ya ndani ili kuweza kugharamia miradi kama hiyo kwa ufanisi zaidi bila kutegemea kwa kiasi kikubwa fedha kutoka Serikali Kuu.

Mradi huu wa jengo la ghorofa ni miongoni mwa juhudi za Halmashauri ya Bunda kubadili sura ya mji huo kwa kuimarisha miundombinu ya kibiashara, kuongeza ajira na kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!