Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, Deodatus P. Mwanyika, ameelekeza Wizara na wadau wa sekta hiyo kuendelea kutathmini mfumo wa stakabadhi ghalani, akisisitiza kuwa biashara isiyo rasmi haina manufaa kwa wakulima na wafanyabiashara.
Kauli hiyo ameitoa wakati wa ziara ya Kamati yake kukagua miradi ya maendeleo mkoani Shinyanga, tarehe 13 Machi 2025 ambapo pia amewataka wadau kufanya mazungumzo ili kuona kama kuna haja ya kuweka bei elekezi kwa mazao kwa maslahi ya wakulima. Pia, amesisitiza juhudi za kutafuta masoko mapya ya mazao, akibainisha kuwa soko la India pekee haliwezi kununua choroko na dengu zote zinazozalishwa nchini.
Kwa upande wake, Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Selemani Jafo, amesema serikali inaendelea kuimarisha mfumo wa stakabadhi ghalani ili kuhakikisha wakulima wananufaika. Amesema kuwa mfumo huo umeleta mafanikio makubwa, ambapo bei ya choroko imeongezeka kutoka Tsh 200-400 hadi Tsh 1,300 kwa kilo.
Dkt. Jafo pia amebainisha kuwa tani takribani 800,000 za mazao mbalimbali zimeuzwa kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani, na kiasi cha shilingi trilioni 2.9 kimepatikana, huku halmashauri zikinufaika kwa mapato ya zaidi ya bilioni 87.
Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala, Bw. Asangye Bangu, amesema kuwa ghala linatakiwa kukidhi vigezo maalum kabla ya kuidhinishwa kufanya kazi chini ya mfumo wa stakabadhi ghalani, ikiwemo kupata elimu na cheti cha uthibitisho.
Ameongeza kuwa wakulima wanaopeleka mazao ghalani hulipwa gharama za usafiri, hatua inayosaidia kupunguza changamoto za usafirishaji wa mazao.
Kwa upande wake, mfanyabiashara wa mazao (Aggregator), Daudi Mpina, ameomba maboresho kwenye mfumo wa malipo, akipendekeza muda wa malipo upunguzwe kutoka saa 48 za sasa hadi saa 24 baada ya mnada ili kuwawezesha wafanyabiashara na wakulima kupata fedha zao haraka.