Latest Posts

BWIGIRI KUPEWA MBINU ZA KULINDA WANAWAKE NA WATOTO WENYE ULEMAVU DHIDI YA UKATILI

Taasisi ya Foundation for Disabilities Hope (FDH) imeanzisha mradi wa miezi sita katika kata ya Bwigiri, mkoani Dodoma kwa lengo la kuzuia ukatili dhidi ya wanawake na watoto wenye ulemavu.

Mradi huu unalenga kuwapa mbinu za kujilinda dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia na kutokomeza mila potofu zinazowakumba wanawake, watoto, na watu wenye ulemavu katika jamii zao.

Mkurugenzi wa FDH, Michael Salali, alitangaza uzinduzi wa mradi huu wakati wa hafla iliyoandaliwa wilaya ya Chamwino. Mradi huu unafadhiliwa na Shirika la Women Fund Tanzania Trust.

Salali alisisitiza kwamba wanawake wenye ulemavu wanakumbana na changamoto zaidi ikiwemo unyanyasaji wa kijinsia kama kubakwa na kupigwa. Alieleza kuwa lengo la mradi huu ni kuwajengea uwezo wanawake na watoto wenye ulemavu ili waweze kutambua haki zao za msingi, kujua jinsi ya kujilinda, na kuwawezesha kutoa taarifa kwenye vyombo vya usalama pindi wanapokutana na vitendo vya ukatili.

“Ni muhimu jamii pia ijue jinsi ya kuishi na watu wenye ulemavu, na kuhakikisha wanashirikishwa katika mipango yote ya maendeleo,” alisema Salali. “Tunatoa elimu ya haki za binadamu ili watu wenye ulemavu waelewe haki zao na jamii pia ipate uelewa kuhusu jinsi ya kuwaunga mkono.”

Salali alisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa wananchi wa kata ya Bwigiri katika kuhakikisha mafanikio ya mradi huu. Katibu wa Msikiti wa Kata ya Bwigiri, Ustadhi Omary Mtambi, alishukuru kwa mradi huu kuanzishwa katika kata yao na kusema kuwa utasaidia viongozi wa dini katika kuangalia ustawi wa makundi yote, ikiwemo watu wenye ulemavu.

“Viongozi wa dini mara nyingi hukumbana na watu wenye mahitaji maalumu, hasa walemavu, wanaokuja kutafuta msaada katika nyumba za ibada. Tunapongeza kwa kuleta mradi huu katika eneo letu na tunaahidi kutoa ushirikiano mkubwa,” alisema Ustadhi Mtambi.

Aliongeza kuwa taasisi ya FDH kwa kushirikiana na serikali imeonesha dhamira ya dhati katika kupinga vitendo vya ukatili katika jamii. Ustadhi Mtambi pia aliipongeza serikali kwa juhudi zake katika kupinga ukatili dhidi ya watu wenye ulemavu nchini.

Mratibu wa mradi huo, Glory Mbowe, aliongeza kwamba mradi utahusisha pia viongozi wa dini, ambao wana jukumu muhimu katika kuwahudumia watu wenye ulemavu.

“Viongozi wa dini watahusishwa katika mradi huu ili waje kuwa sehemu ya juhudi za kuzuia ukatili dhidi ya wanawake na watoto,” alisema Mbowe.

Mradi huu unatarajiwa kutoa mwanga mpya katika juhudi za kupinga ukatili dhidi ya wanawake na watoto wenye ulemavu, huku ukilenga kuboresha hali ya maisha ya makundi haya muhimu katika jamii ya Bwigiri.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!