Na Josea Sinkala, Mbeya.
Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Mbeya vijijini kimeanza ziara ya kukagua miradi ya maendeleo katika kata kadhaa za wilaya hiyo kwa maslahi ya jamii.
Ziara hiyo ya kamati ya siasa imeongozwa na Katibu wa CCM Wilaya (Mbeya Vijijini – kichama) Rehema Hosea Mpagike ziara ambayo inafanyika kwa muda wa siku tatu mfululizo.
Kamati ya siasa mnamo Mei 12, 2025 imetembelea na kukagua miradi ya maendeleo katika Kata ya Ulenje hasa kituo cha Afya kinachoendelea kujengwa kwa nguvu za wananchi, mfuko wa jimbo na fedha kutoka Serikalini.
Baada ya kata ya Ulenje, Kamati ya siasa Wilayani humo, imetembelea na kukagua ujenzi wa Zahanati ya kijiji cha Mwanzazi Kata ya Igoma pamoja na mradi wa ujenzi wa bweni katika shule ya Sekondari ya wasichana Galijembe iliopo Kata ya Tembela Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya ambapo wajumbe wa kamati hiyo wameeleza kuridhishwa na utekelezwaji wa miradi mbalimbali inayoendelea kutekelezwa na Serikali.
Katibu wa CCM Wilaya ya Mbeya vijijini na wajumbe wa kamati ya siasa wamempongeza Mkuu wa Wilaya ya Mbeya Mhe. Beno Moris Malisa kwa usimamizi mzuri wa miradi inayoendelea kutekelezwa na Serikali katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya.
Ziara hiyo iliyoanza mei 12, 2025 inatarajiwa kuendelea kwa muda wa siku tatu hadi Mei 14, 2025 ambapo CCM kama ilivyo wajibu wake mkuu itatembelea na kukagua miradi mbalimbali, kushauri na kutoa maelekezo mahali panapoonekana kuwa na tatizo ili kuhakikisha miradi inaendana na thamani halisi ya fedha za wananchi na Serikali kwa maslahi mapana ya jamii.