Kamati ya siasa ya mkoa wa Ruvuma imezishauri halmashauri zote za mkoa huo kuwasiliana na Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ili kuangalia upya utaratibu wa utoaji fedha za miradi inayosimamiwa na wizara hiyo, kwa kuzingatia mazingira halisi ya maeneo husika.
Ushauri huo umetolewa kufuatia kuwepo kwa changamoto ya baadhi ya halmashauri kushindwa kukamilisha miradi ya maendeleo kutokana na makadirio ya fedha kuwa madogo, pamoja na gharama kubwa za usafirishaji wa vifaa vya ujenzi vinavyopatikana mbali na maeneo ya miradi.

Akizungumza wakati wa ukaguzi wa ujenzi wa bwalo la chakula katika Shule ya Sekondari Masonya iliyopo wilayani Tunduru, Katibu wa Siasa na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Ruvuma, ndugu John Foroteo Haule, amesema miradi mingi inayotekelezwa kupitia TAMISEMI inakabiliwa na changamoto ya kutokamilika kwa wakati kutokana na upungufu wa fedha.
Amesema hali hiyo inachangiwa kwa kiasi kikubwa na umbali wa upatikanaji wa vifaa vya ujenzi, hali inayosababisha sehemu kubwa ya fedha za miradi kutumika katika usafirishaji badala ya ujenzi wenyewe.
Kutokana na hali hiyo, ameongeza kuwa baadhi ya halmashauri zimelazimika kutumia mapato yao ya ndani kukamilisha miradi ya TAMISEMI, jambo ambalo linaathiri utekelezaji wa mipango mingine ya maendeleo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Shule ya Sekondari Masonya, Mwalimu Macrina Ngonyani, amesema shule hiyo imepokea shilingi milioni 168 kwa ajili ya ujenzi wa bwalo la chakula lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 400.

Amesema hadi sasa jumla ya shilingi milioni 165.7 zimetumika na ujenzi umefikia hatua ya umaliziaji, huku kiasi kilichobaki cha shilingi milioni 2.3 kikiwa hakitoshi kukamilisha mradi