Viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Temeke wamefanya ziara maalum wilayani Bagamoyo, Mkoa wa Pwani, kwa lengo la kujifunza na kuhifadhi historia ya harakati za ukombozi wa Tanzania tangu enzi za Chama cha TANU hadi kuundwa kwa CCM.
Ziara hiyo, ambayo ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 48 ya CCM, iliwapeleka viongozi hao kwenye maeneo muhimu ya kihistoria, ikiwemo sehemu alikowahi kufikia Mwalimu Julius Nyerere wakati wa harakati za kupigania uhuru wa Tanganyika.
Akizungumza baada ya ziara hiyo, Katibu wa Vyuo na Vyuo Vikuu wa CCM Temeke, Dua Mkoga, alisema wameamua kwenda Bagamoyo kwa sababu ni sehemu yenye alama muhimu za harakati za ukombozi wa taifa.

“Tumejifunza hatua walizopitia waasisi wa TANU na CCM katika harakati za ukombozi wa nchi yetu. Tutaendelea kutumia historia hii kuboresha utendaji wetu, hasa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu,” alisema Mkoga.
Kwa upande wake, Katibu wa Siasa na Uenezi wa Kata ya Temeke, Innocent Mahendeka, alitaja maeneo muhimu waliyotembelea, yakiwemo:
✅ Ofisi za CCM Wilaya ya Bagamoyo
✅ Shina la CCM lililoanzia TANU (Mti Pesa)
✅ Jengo la Ikulu ya Kwanza ya Afrika Mashariki
✅ Magofu ya Kaole na historia ya machifu
✅ Mnara wa TANU, eneo ambalo Nyerere alikutana na Shehe Ramiya
✅ Mji Mkongwe wa Bagamoyo na vivutio vya utalii
Mzee Mwinyi Akida, mmoja wa wazee wa Bagamoyo, alisimulia jinsi Mwalimu Julius Nyerere alivyofika Bagamoyo mwaka 1954 na kukutana na wazee wa mji huo kuwaeleza azma yake ya kupigania uhuru wa Tanganyika.

“Nyerere alikutana na Shehe Lamia, ambaye alimshauri wafanye dua maalum wakiwa wamefunga kwa siku moja. Nyerere alikubali, na dua hiyo ilifanyika kumuomba Mwenyezi Mungu afanikishe harakati zake za kutuletea uhuru,” alisema Mzee Akida.
Baada ya dua hiyo, Mwalimu Nyerere aliendelea na safari zake za harakati, akifanya mikutano mbalimbali kueleza dhamira yake ya kuikomboa Tanganyika kutoka kwa wakoloni.
Katibu wa Jukwaa la Wanawake wa CCM Kata ya Azimio, Victoria Charles, alisema ziara hiyo pia ilikuwa sehemu ya kumuenzi Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake za kuendeleza maendeleo kupitia CCM.
“Tumepata picha kamili ya jinsi Mwalimu Nyerere alivyopambana kuleta uhuru wa nchi hii. Tutaendelea kuwaeleza wanachama wa CCM na wananchi wengine umuhimu wa kutembelea Bagamoyo ili kuelewa historia ya taifa letu,” alisema Victoria.
Katika ziara hiyo, viongozi wa CCM Temeke walipata fursa ya kushuhudia miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa chini ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ikiwa ni mwendelezo wa maono ya waasisi wa taifa hili.
