Na Josea Sinkala, Mbeya.
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) jimbo la Lupa wilayani Chunya mkoani Mbeya, kimehitimisha zoezi la urejeshaji fomu za kugombea nafasi mbalimbali za uongozi kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa, vitongoji na vijiji baadaye mwaka huu (2024).
Akizungumza mjini Chunya, Katibu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo jimbo la Lupa (Chunya) Yohana Mpamba (Mcotton), amesema CHADEMA imekamilisha mchakato wa kurudisha fomu katika ofisi za vijiji mbalimbali wakihitimisha katika kata mbili za Itewe na Chokaa Chunya Mjini na kuahidi kuhamasisha wananchi kujitokeza kupiga kura kuhakikisha CHADEMA inashinda.
“Ndugu zangu wanachama wote, watia nia na wananchi nawashukuru sana kwa kujitokeza kutusindikiza kuhamasisha urejeshaji wa fomu za kugombea kwa viongozi wetu, ninachotaka tu niwaambie zoezi limeenda vizuri tangu kuchukua fomu na kurejesha, changamoto zikikuwepo ndogondogo lakini namshukuru msimamizi wa uchaguzi wilaya (Mkurugenzi wa Halmashauri ya Chunya Tamimu Kambona) kwani tulikuwa tukikutana na changamoto tunaisuluhisha mapema kwahiyo CHADEMA tunaamini wagombea wetu wote kama ambavyo zoezi limeenda vizuri basi naamini fomu zao zitapokelewa na watapitishwa wote na tutashinda na tuache kulialia”, amesema katibu wa CHADEMA jimbo la Lupa.
Hata hivyo Mcotton amewataka wanachama wa Chama hicho kwenda kuwashawishi wenzao kujitokeza kwa wingi kwenye mikutano yao ya kampeni na kuhimiza wananchi kujitokeza kupiga kura kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa, vitongoji na vijiji Novemba 27, 2024 kwa kuchagua viongozi bora kupitia CHADEMA akisema watakwenda kusimamia maslahi ya wananchi kwa maendeleo yao.
Wagombea mbalimbali wa CHADEMA katika nafasi za vijiji, ujumbe wa vijiji na vitongoji wamesema wako tayari kwenda kushinda kwenye uchaguzi ujao na kuwaomba wananchi kuwaamini kwenye uchaguzi huo.
Ikumbukwe kuwa uchaguzi wa Serikali za mitaa, vitongoji na vijiji unatarajiwa kufanyika Novemba 27, 2024.