Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimetangaza kuwa Jumanne, Machi 18, 2025, kitaonana na Msajili wa Vyama vya Siasa jijini Dar es Salaam kujadili ajenda yao ya mageuzi ya uchaguzi kupitia Kaulimbiu yao ya “No Reforms, No Election”, ikisisitiza msimamo wa chama kuhusu mabadiliko ya mfumo wa uchaguzi kabla ya kushiriki katika uchaguzi ujao.
Kulingana na taarifa iliyotolewa Jumatatu Machi 17, 2025 na Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi wa chama hicho Brenda Rupia, Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika ataongoza ujumbe wa chama katika kikao hicho ambacho kikimalizika tu, chama kitatoa mrejesho rasmi kwa wanachama na umma kwa ujumla.