Latest Posts

CHADEMA SHINYANGA YATANGAZA USHIRIKI MAANDAMANO YA AMANI DAR ES SALAAM SEPTEMBA 23

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mkoa wa Shinyanga kimetoa tamko rasmi la kuunga mkono wito uliotolewa na Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho, Freeman Mbowe, kuhusu maandamano ya amani yaliyopangwa kufanyika jijini Dar es Salaam mnamo Septemba 23, 2024.

Uongozi wa CHADEMA Shinyanga, ukiongozwa na Mwenyekiti wa mkoa, Chief Ntobi, umetoa wito kwa wanachama na wafuasi wote wa chama kujiandaa na kuhudhuria maandamano hayo ambayo yanalenga kulinda uhai na kupinga vitendo vya utekaji na mauaji vinavyoendelea nchini.

Katika taarifa yake kwa umma iliyotolewa tarehe 13 Septemba 2024, Chief Ntobi ameeleza kuwa chama hicho mkoani Shinyanga kimeamua kuunga mkono azimio lililotolewa makao makuu ya CHADEMA jijini Dar es Salaam mnamo Septemba 11, 2024.

“Tunawaagiza viongozi wetu wote wa wilaya, majimbo, kata, matawi na misingi kuanza maandalizi mara moja kwa ajili ya safari ya kuelekea Dar es Salaam kwenye kazi hii maalumu ya chama,” amesema Ntobi.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, CHADEMA Shinyanga imejipanga kuhakikisha ushiriki mkubwa wa wanachama kutoka maeneo yote ya mkoa huo.

“Tutahakikisha wanachama na wafuasi wetu kutoka wilaya zote tatu, majimbo yote sita, kata zote 130, matawi yote 506, na misingi yote 2938 wanashiriki katika maandamano haya ya amani,” ameongeza Ntobi.

Ntobi amesisitiza kuwa maandamano hayo ni ya amani na yaliyo na lengo la kulinda usalama wa raia na kupinga matendo ya kinyama yanayofanyika nchini. Alisema kuwa wanachama wa CHADEMA Mkoa wa Shinyanga wanatakiwa kutumia usafiri wa umma na kuepuka kuvaa mavazi ya chama ili kuepuka ucheleweshaji wa safari njiani.

“Wakati wa safari, watu wetu watumie usafiri wa umma na wasiwe wamevaa nguo za chama. Hii ni kuepusha kucheleweshwa njiani na hao wasiokuwa na uchungu na matendo ya utekaji yanayoendelea nchini,” ameeleza.

Aidha, Ntobi ameonesha masikitiko makubwa kutokana na kuendelea kushuhudiwa kwa matukio ya utekaji, mateso, na mauaji ya wanachama wa chama hicho na wananchi kwa ujumla.

CHADEMA Mkoa wa Shinyanga imeweka wazi kuwa itaungana na wanachama wa mikoa mingine nchini katika kuhakikisha maandamano hayo yanafanyika kwa amani, huku ikiwa na lengo la kudai haki na kuimarisha usalama wa wananchi, na si kuchochea vurugu au hofu.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!