Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kanda ya Victoria kimesema kimejipanga kuchukua hatua kali dhidi ya wagombea wake ambao watakubali kurubuniwa katika uchaguzi wa serikali za mitaa kutokana na viashiria vya urubuni ambavyo tayari vimeanza kujitokeza.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa CHADEMA Kanda ya Victoria, Ezekia Wenje, amesema chama hicho hakiko tayari kuona mgombea wake yeyote aliyeteuliwa na kupewa fomu anarubuniwa.
Ameeleza kuwa msimamo wa chama ni kuwachukulia hatua wagombea wote watakaokubali kurubuniwa ili wasishiriki katika uchaguzi huo.
Wenje amebainisha kuwa tayari katika kanda hiyo, mgombea mmoja wa jimbo la Sumve amerubuniwa na kuandika barua ya kujiondoa katika uchaguzi huo. Amesema CHADEMA imewaagiza wanachama wake jimboni humo kumchukulia hatua mgombea huyo kama fundisho kwa wengine.
Kwa upande wake, Katibu wa CHADEMA mkoa wa Mwanza, Boniphase Nkobe, amesema baadhi ya wasimamizi wa uchaguzi katika mkoa huo, ikiwemo wa Jimbo la Buchosa, wamekuwa wakiwazuia wasaidizi wa uchaguzi kutoa nakala. Nkobe ameonya kuwa kama vitendo hivyo vitaendelea, CHADEMA inaweza kuchukua hatua ya kuwakataa wasimamizi hao kwa kuonekana kuvuruga uchaguzi.