Shughuli ya utiaji saini wa Kanuni za Maadili ya Uchaguzi kwa ajili ya uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu, imefanyika rasmi leo, Aprili 12, 2025, jijini Dodoma, bila ushiriki wa chama kikuu cha upinzani nchini, CHADEMA.
Hafla hiyo iliyoandaliwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), ilihusisha vyama vyote vya siasa vyenye usajili wa kudumu, Serikali, na Tume yenyewe kwa lengo la kukubaliana na kusaini kanuni zitakazosimamia mchakato wa uchaguzi huo.
Katika ukumbi wa tukio hilo, vyama vilipangiwa viti kwa kufuata nafasi za makatibu wakuu. Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika, alitarajiwa kuketi katikati ya Katibu Mkuu wa CCM, Dkt. Emmanuel Nchimbi na Katibu Mkuu wa CHAUMMA, Mohamed Rashid — lakini kiti hicho kilibaki wazi, na hali hiyo kuibua maswali kutoka kwa waandishi wa habari na waangalizi wa uchaguzi.
Mwenyekiti wa INEC, Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele, alipokuwa akivitaja vyama kimoja baada ya kingine kuthibitisha kukubaliana na kusaini kanuni hizo, alielezwa kuwa Chadema hawapo. Mkurugenzi wa Uchaguzi, alipoulizwa kuhusu hilo, alithibitisha kuwa alizungumza na Katibu Mkuu wa Chadema ambaye alisema rasmi kuwa chama hicho hakitafika kusaini.
Vyama vilivyoshiriki hafla hiyo ni pamoja na CCM, CUF, ACT-Wazalendo, CHAUMMA, TLP, NCCR-Mageuzi, UDP, CCK, ADC, Demokrasia Makini, DP, NRA, NLD, SAU, UDPD, ADA-TADEA, AAFP na UMD.
Kutokuwepo kwa Chadema katika hatua hii muhimu ya maandalizi ya uchaguzi kunazidi kuibua sintofahamu juu ya msimamo wa chama hicho kuelekea uchaguzi mkuu, ambapo mpaka sasa bado kimeshikilia msimamo wake wa kutoshiriki uchaguzi bila mabadiliko ya msingi ya mfumo wa uchaguzi, wakisisitiza kauli yao ya No Reforms, No Election.
Kwa mujibu wa taratibu za Tume ya Uchaguzi, chama ambacho hakitasaini Kanuni za Maadili ya Uchaguzi hakitaruhusiwa kushiriki kwenye uchaguzi huo, jambo ambalo linaiweka Chadema katika nafasi tata kisiasa ikiwa hakutakuwa na suluhu ya haraka.