Latest Posts

CHADEMA: ZUIO LA SISI KUFANYA SIASA LILIKOMA DESEMBA 10, POLISI ACHENI KUINGILIA SHUGHULI ZETU

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimetoa taarifa rasmi kwa umma kikibainisha kuwa amri ya zuio la Mahakama Kuu iliyokuwa ikikizuia chama hicho kufanya shughuli za kisiasa nchini imekoma kisheria tangu tarehe 10 Desemba, 2025.

Katika taarifa iliyotolewa leo, Januari 23, 2026, na Mwanasheria Mkuu wa CHADEMA, Dkt. Rugemeleza Nshala, chama hicho kimesema kuwa amri hiyo iliyotolewa na Jaji Hamidu Mwanga mnamo tarehe 10 Juni 2025, ilikuwa na ukomo wa miezi sita kwa mujibu wa Sheria ya Mwenendo wa Madai (Civil Procedure Code).

Dkt. Nshala amefafanua kuwa, kwa mujibu wa Kanuni ya 3 ya Amri ya 37, amri yoyote ya zuio la muda haiwezi kuzidi miezi sita isipokuwa kama kuna maombi ya ziada ya kuiongeza, jambo ambalo halikufanyika.

“Ikiwa ni pamoja na masharti mengine ya kutunza hesabu na kutoa amana, Mahakama inaweza kutoa amri ya zuio kwa mujibu wa kanuni ya 1 au kanuni ya 2 na amri hiyo itakuwa na maisha kwa kipindi kilichotajwa na Mahakama, lakini kisichozidi miezi sita…Kifungu hiki cha sheria kilitafsiriwa kwa utuo na Mahakama ya Rufaa ya Tanzania katika kesi ya African Trophy Hunting Ltd vs Attorney General and 4 Others (Civil Appeal 25 of 1997) [1998] TZCA 11 (3 December 1998), ambapo Mahakama hiyo ya juu kabisa nchini ilisema kwa uwazi kabisa kuwa amri ya zuio inaweza kutolewa kwanza kwa miezi sita na inaweza kuongezwa zaidi lakini nyongeza hiyo ikiwa ni pamoja na zuio la kwanza lisizidi jumla ya mwaka mmoja”, imeeleza taarifa hiyo.

Taarifa hiyo imekuja kufuatia matukio ya hivi karibuni ambapo Jeshi la Polisi mkoani Mbeya (Mbalizi) na mkoani Rukwa (Nkasi) liliingilia shughuli za chama hicho. Mkoani Mbeya, polisi walielezwa kuvamia ofisi ya CHADEMA tawi la Inyala na kushusha bendera iliyokuwa nusu mlingoti kuomboleza kifo cha muasisi wa chama hicho, Mzee Edwin Mtei, hatua ambayo polisi walisema chama hicho kilifanya mkusanyiko usio halali na kilikiuka zuio la mahakama. Kule Nkasi, wanachama walizuiliwa kufanya zoezi la upandaji miti la kuadhimisha miaka 33 ya usajili wa chama hicho, hata hivyo polisi walikana kutumia nguvu yoyote katika tukio hilo.

“Hivyo kitendo cha Polisi kushusha bendera ya CHADEMA wilayani Mbeya Vijjini ulikuwa ni uvunjifu mkubwa wa sheria kama vile ilivyo kwa kitendo cha Jeshi la Polisi kuzuia wanachama kufanya kazi zao za kisiasa ikijumuisha maadhimisho ya miaka 33 ya kusajiliwa rasmi kuwa chama cha siasa nchini. Aidha, kesi iliyofunguliwa na hao wanachama mamluki dhidi ya CHADEMA ni ya madai na hivyo Polisi hawana mamlaka ya kudai kuitekeleza isipokuwa tu pale kunapokuwa na amri nyingine ya Mahakama inayowaamuru kutekelezwa kwayo kutokana na maombi ya kuwakuta wale wanaodaiwa kuikiuka kuwa wametiwa hatiani na Mahakama kwa kosa la kudharau amri ya mahakama”, ameeleza Dkt. Nshala.

CHADEMA imetoa onyo kali kwa maofisa wa polisi na watumishi wa umma wanaotumia kisingizio cha zuio hilo lililokoma kuingilia haki zao za kikatiba. Imesema haitasita kumfungulia mashtaka ya binafsi ofisa yeyote atakayezuia shughuli zao, ikijumuisha kudai fidia ya kifedha na kuomba mahakama itamke kuwa ofisa huyo hana sifa ya kuendelea kuwa mtumishi wa umma.

“CHADEMA ni chama kilichosajiliwa kihalali nchini chenye haki ya kufanya shughuli zake za kisiasa nchini kote, Jeshi la Polisi lazima lifahamu haliko juu ya sheria na halina mamlaka ya kusimamisha au kupoka haki za vyama vya siasa, wanachama wake na wananchi kwa ujumla nchini kufanya shughuli za siasa. Hakuna zuio lolote lile la Mahakama Kuu juu ya kutenda shughuli za kisiasa kwani amri yake ya tarehe 10 Juni 2025 ilikoma tarehe 10 Desemba 2025”, imeelezwa katika taarifa hiyo.

CHADEMA imewataka viongozi na wanachama wake nchi nzima kuendelea na shughuli za kisiasa kama kawaida, huku ikiwataka kutoa taarifa mara moja Kurugenzi ya Sheria na Katiba ya chama hicho iwapo watakumbana na kizuizi chochote kisicho cha kisheria.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!