Latest Posts

CHANGAMOTO ZA MAREJESHO ZAAINISHWA MKOPO WA IMBEJU UKIENDELEA KUNUFAISHA WANAWAKE TARIME

Na Helena Magabe, Tarime

‎IMBEJU ni mkopo wezeshi usio na riba unaotolewa na Benki ya CRDB kwa ajili ya wanawake na vijana. Hata hivyo, kwa Wilaya ya Tarime, mkopo huu umejikita zaidi kuwawezesha wanawake. Mpaka sasa, zaidi ya akaunti 500 za vikundi vya wanawake zimefunguliwa, ambapo wanawake ndio wameendelea kunufaika zaidi.

‎Afisa Mahusiano wa CRDB, Mafulu Sebastian, ameeleza kuwa mkopo huo unatolewa kwa vijana na wanawake kupitia vikundi vilivyosajiliwa na vilivyodumu kwa angalau miaka miwili. Amesema mkopo huo unaanzia shilingi 200,000 hadi 5,000,000, hauna riba, na marejesho yake hufanyika ndani ya mwaka mmoja.

‎Sebastian amebainisha kuwa pamoja na kuwa mkopo huo unalenga wanawake na vijana, wanawake wamepewa kipaumbele zaidi kutokana na jinsi wanavyowajibika. Amesema, “Wanawake wamekuwa wakifuatilia zaidi mkopo huu, na wengi wao ni wajasiriamali wadogo kama wauza dagaa na wengineo.”

‎Hata hivyo, amefafanua kuwa vijana kwa sasa hawapewi kipaumbele kutokana na kutokuwa makini  katika marejesho ya mikopo. “Benki yetu ni ya biashara. Tunawakopesha wanawake, lakini hata wao wameanza kuwa wasumbufu kwenye marejesho. Ukimpigia mtu simu anakwambia biashara ni mbaya – kila siku biashara ni mbaya, Kila siku afungua biashara lakini  wanapohitaji mkopo wanashinda humu ndani,” amesema.

‎Sebastian ameeleza kuwa mkopo huo hutolewa kupitia vikundi, na kabla ya kupatiwa mkopo, wanatakiwa kuweka asilimia 10 ya kiasi wanachoomba kwenye akaunti zao za IMBENJU. Benki hufunga kiasi hicho hadi pale kikundi kinapokamilisha marejesho ndipo pesa hiyo hufunguliwa.

‎Pamoja na mafanikio yaliyopatikana, amesema changamoto kubwa imekuwa kwenye marejesho. “Elimu ya fedha iko chini. Pengine kwa sababu walizoea mikopo ya ‘kausha damu’ ambapo walikamatiwa mali, sasa kwa kuwa sisi hatufanyi hivyo, na fomu za mkopo hazionyeshi kukamaitiwa mali sisi benki hatuna utaratibu huo Mpaka tufikie hatua ya kuchora nyumba kwamba inauzwa, ina maana tumevumilia sana,” amesisitiza.

‎Kutokana na usumbufu, ameeleza kuwa kiwango cha juu cha mkopo kimeshushwa kutoka milioni tano hadi milioni nne. Hivi sasa, mkopo huo unaanzia shilingi 1,500,000 hadi 4,000,000. Aidha, waombaji wa mkopo watachujwa zaidi, na watakaoendelea kukopeshwa ni wale tu wasiosumbua katika marejesho.

‎“IMBEJU ina mambo mawili: mwanakikundi na kikundi. Wote wanatakiwa kuwa na kadi maalum ya IMBEJU hata kama tayari wana kadi ya kawaida ya CRDB,” ameeleza.

‎Mmoja wa wanufaika wa mkopo wa IMBEJU, ambaye hakutaka jina lake litajwe, amesema mkopo huo umeinufaisha wanawake wengi, lakini baadhi yao wamekuwa wagumu kwenye marejesho, hata kuanzia rejesho la kwanza.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!