Taasisi ya Utafiti na Utetezi wa Haki za Ardhi (HAKIARDHI), kwa kushirikiana na mashirika mengine yasiyo ya kiserikali, imetangaza Kongamano la Kitaifa la Masuala ya Ardhi litakalofanyika tarehe 28 na 29 Oktoba 2024 katika Hoteli ya Stella Maris, Bagamoyo, litakalojadili masuala muhimu yanayohusiana na haki za ardhi, usimamizi wa rasilimali, na kutafuta suluhisho la migogoro inayokumba jamii za wakulima, wafugaji, na wazalishaji wadogo.
Katika tukio hilo, HAKIARDHI pia itasherehekea miaka 30 tangu kuanzishwa kwake mwaka 1994. Akizungumza na waandishi wa habari siku ya Jumanne Oktoba 22, 2024, Mkurugenzi Mtendaji wa HAKIARDHI, Cathbert Tomitho, ameeleza kuwa kongamano hili linafanyika wakati ambapo taifa linaendelea kukabiliana na changamoto nyingi zinazohusiana na ardhi, hasa migogoro ya mara kwa mara kati ya wakulima na wafugaji, wawekezaji na jamii, pamoja na matatizo ya usimamizi wa ardhi mijini na vijijini.
“Ardhi ni uhai wa taifa letu na nyenzo kuu ya uzalishaji mali. Bila usimamizi bora wa ardhi, uchumi wetu na maisha ya wazalishaji wadogo yako mashakani,” amesema Tomitho.
Ameongeza kuwa kongamano hilo litakuwa fursa muhimu kwa wadau kutoa maoni na mapendekezo yatakayosaidia kuimarisha mfumo wa usimamizi wa ardhi nchini, hususan kwa wazalishaji wadogo ambao ndio uti wa mgongo wa uchumi wa Tanzania.
Pamoja na kujadili mada kuu kuhusu mfumo wa umiliki wa ardhi nchini, kongamano hilo litatoa nafasi ya kufanya tathmini mpya kuhusu vyama vya ushirika vya wazalishaji wadogo, kuharakisha utekelezaji wa maamuzi yanayowahusu wazalishaji wadogo, na kuchambua uporaji wa ardhi katika muktadha wa uhifadhi wa wanyamapori na uwekezaji wa kilimo biashara.
Tomitho ameeleza kuwa kongamano hili litajadili kwa kina jinsi ambavyo ardhi ya kijiji, hasa katika maeneo ya uzalishaji wa chakula, inavyohitaji ulinzi dhidi ya kupanuka kwa hifadhi za wanyamapori, miji, na athari za mabadiliko ya tabianchi.
“Kwa miaka 30 sasa, HAKIARDHI imekuwa ikifanya kazi kwa karibu na jamii za vijijini kuhakikisha kuwa haki zao za ardhi zinalindwa na kwamba ardhi haiwi bidhaa inayouzika kiholela. Tunahitaji mfumo wa sheria na sera unaozingatia maslahi ya wazalishaji wadogo,” amesema Tomitho.
Ametoa wito kwa serikali kuendelea kutekeleza mapendekezo ya Tume ya Rais ya Uchunguzi wa Masuala ya Ardhi ya mwaka 1991, yaliyosisitiza umuhimu wa kupunguza mamlaka makubwa ya serikali katika usimamizi wa ardhi na kuimarisha mamlaka za wananchi kama Mkutano Mkuu wa Kijiji na Halmashauri za Vijiji.
Katika maadhimisho haya ya miaka 30, HAKIARDHI itaweka msisitizo juu ya ulinzi wa ardhi ya kijiji, ambayo imekuwa ikipungua kwa kasi kutokana na kuongezeka kwa shughuli za uhifadhi wa wanyamapori na upanuzi wa miji. Taasisi hiyo pia itaendelea kupigania kuwa na sura mahsusi ya ardhi, rasilimali, na mazingira katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kuimarisha ulinzi wa ardhi na rasilimali nyingine muhimu kwa ustawi wa jamii.
Taarifa kutoka HAKIARDHI pia zimeeleza kuwa Sheria za Ardhi za mwaka 1999, pamoja na sera ya ardhi ya mwaka 1995, bado zinakabiliwa na changamoto kubwa katika utekelezaji wake, hususan kutokana na ongezeko la migogoro ya ardhi nchini. Kongamano hili linatarajiwa kutoa mwanga zaidi kuhusu hatua ambazo serikali inapaswa kuchukua ili kuhakikisha ardhi inakuwa nyenzo ya maendeleo kwa wananchi wote.
Tomitho alimalizia kwa kutoa wito kwa wadau wote wa ardhi kushiriki kikamilifu katika kongamano hili ili kujadili kwa kina masuala yanayohusu haki za ardhi na usimamizi wake, huku akiweka bayana kuwa “Ardhi sio bidhaa, bali ni uhai” na inapaswa kutumika kwa maslahi ya wote.
Kongamano hilo litawaleta pamoja wadau wapatao 200 kutoka sekta ya ardhi nchini, ikiwa ni pamoja na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Tume ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi, Wizara ya Kilimo, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, wakulima, wafugaji, na mashirika yasiyo ya kiserikali.