Na Josea Sinkala, Mbeya.
Chama cha Ukombozi wa Umma Tanzania (CHAUMMA) mkoa wa Mbeya kimesema awamu hii kinafanya kampeni za uchaguzi wa Serikali za mitaa kidigitali tofauti na ilivyozoeleka na vyama vingine.
Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa Chama hicho mkoa wa Mbeya Ipyana Samson Njiku wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Mbeya ambapo amesema chama chake hakina raslimali fedha hivyo wamepanga kutumia vipaza sauti kwenye kampeni ili kuwafikia wapiga kura na kuomba wawachague wagombea wake.
Njiku, amewaomba wananchi kukiunga mkono chama hicho kwa kuwachagua wagombea wake wa nafasi mbalimbali na kueleza kipaumbele cha CHAUMMA kuwa ni kukabiliana na mmomonyoko wa maadili ambao viongozi wa Serikali za mitaa, vitongoji na vijiji wana nafasi kubwa kwa kutunga sheria ndogondogo kuanzia ngazi za mitaa, vitongoji na vijiji bila kuacha suala la lishe ambayo ni kampeni yao endelevu.
Pamoja na hayo, ameeleza kukerwa na baadhi ya matendo maovu yanayofanyika mitaani ikiwemo ubakaji na ukatili wa kijinsia ambavyo amedai baadhi hufumbiwa macho na viongozi wa ngazi hizo za chini wasiokuwa waadilifu.
Ikumbukwe kampeni za uchaguzi wa Serikali za mitaa, vitongoji na vijiji zilianza tangu Novemba 20, 2024 na zitatamatika Novemba 26, 2024 kisha uchaguzi kufanyika Novemba 27 2024 ambapo sasa vyama mbalimbali vya siasa vinaendelea kunadi sera zao kwa wananchi wakiomba kuchaguliwa.