Na; mwandishi wetu
Siku moja baada ya Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA) kufanya uzinduzi wa oparesheni ‘CHAUMMA For Change -C4C’ kwenye uwanja wa Furahisha, jijini Mwanza leo, Jumatano Juni 04.2025 chama hicho kimeachia picha rasmi zinazoonesha namna umati wa watu walivyojitokeza kwenye uwanja huo wakati wa mkutano wa hadhara
Kuachiwa kwa picha hizo, kunakuja kufuatia kuibuka kwa mjadala ‘hasi’ dhidi ya chama hicho hususani kwenye mitandao ya kijamii ikionesha kuwa huenda wakazi wa jiji la Mwanza walisusia mkutano huo na hivyo hawakujitokeza kwa uwingi wake tofauti na ilivyotarajiwa jambo ambalo si sahihi
Katika mkutano huo wa hadhara uliodhuriwa na viongozi waandamizi wa CHAUMMA wakiongozwa na Mwenyekiti wake wa Taifa Wakili Hashim Rungwe Spunda (Mzee wa Ubwabwa), Kaimu Makamu Mwenyekiti Tanzania Bara Devotha Minja, Katibu Mkuu Salum Mwalimu, Naibu Katibu Mkuu Tanzania Bara Benson Kigaila na wengineo, Jambo TV imeona picha zilizoachiwa na chama hicho, baadhi ya picha hizo zikiwa zimeambatanishwa kwenye habari hii ambapo kwa ujumla picha hizo zinaonesha ‘mamia kwa maelfu’ ya wananchi waliojitokeza kwenye mkutano huo
Kilichokuwa kinashuhudiwa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii inaweza kuwa ni sehemu ya propaganda ambayo mara kadhaa imekuwa ikishuhudiwa kuhusu chama hicho, na pengine wale wasiokitakia mema walitumia ajenda hiyo ‘kupush’ picha ambazo si sahihi na sio rasmi ili kuuaminisha umma kuwa pengine mkutano huo ‘ulidorora’ jambo ambalo si sahihi
Miongoni mwa picha jongefu (Video) inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii kuhusiana na tukio hilo la Juni 03.2025 ni ile inayomuhusisha Naibu Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Sheria na Haki za Binadamu CHAUMMA Esther Fulano ambaye aliueleza umma kupitia mkutano huo kwa namna gani chama hicho kimejizolea maelfu ya wafuasi waliojitokeza kusikiliza
“Ahsanteni sana wana Mwanza kwa kutuunga mkono, kuna mtu alisema mkifika watu elfu 30 uwanjani nahama nchi, mfikishieni habari kwamba tuko wengi sana, kwa mara ya kwanza CHAUMMA tuko wengi sana uwanjani” -Esther
Hata hivyo, video hiyo ilipokelewa kwa hisia mseto kwenye mitandao ya kijamii wengi wakidai kuwa kile alichokuwa anazungumza hakina uhalisia wowote, kitendo cha CHAUMMA kuachia picha rasmi na sahihi za mkutano huo sio tu ‘kinaziba midomo’ lakini pia kinaonesha namna kilivyoamua kujibu kwa vitendo na kuonesha uhalisia wake.