Latest Posts

CUF MBEYA: UPINZANI TUUNGANE, 2025 TUSHINDE NA KUKOMESHA UTEKAJI

Na Josea Sinkala, Mbeya.

Katibu wa Chama cha Wananchi (CUF) mkoa wa Mbeya Ibrahim Mwakwama, amesema wapinzani wanatakiwa kuachana na maslahi binafsi badala yake waungane ili kuhakikisha uchaguzi mkuu ujao wa 2025 wanashinda hususani ubunge na udiwani mkoani Mbeya ili kuwaletea maendeleo ya kweli wananchi.

Kiongozi huyo amesema hayo wakati wa mazungumzo yake kuhusu masuala mbalimbali ya siasa za Tanzania, maendeleo ya mkoa wa Mbeya na Tanzania kwa ujumla, sanjari na maandalizi ya uchaguzi mkuu wa 2025.

Amesema chama chake kimejiandaa kuhakikisha uchaguzi ujao unakuwa wa ushindani kwani wameazimia kuungana na vyama vingine vinane vya upinzani mkoani Mbeya isipokuwa CHADEMA kuhakikisha kwa pamoja wanasimamisha mgombea ubunge atakayekuwa hitaji la Wanambeya Mjini ili kufanikisha kumuondoa madarakani kupitia sanduku la kura Mbunge wa Mbeya Mjini Dkt. Tulia Ackson ambaye ndiye Spika wa Bunge la Tanzania akidai jiji la Mbeya limedumaa kimaendeleo.

Aidha Ibrahim Mwakwama, ameeleza kukerwa na sintofahamu na migongano anayoitaja kuwa ni ya kimaslahi miongoni mwa vyama vya wapinzani akigusia suala la wenyeviti Taifa wa CHADEMA na CUF ambao ni Freeman Aikael Mbowe na Mwenyekiti wa CUF Taifa Prof. Ibrahim Haruna Lipumba, kuendelea kusalia madarakani akidai wangeacha nafasi kwa wengine badala ya kukaa nafasi za juu kwa muda mrefu hivyo kutorusu mabadiliko akiwaita kuwa ni akina ‘Nkurunzinza (Rais wa zamani wa Burundi)’ waliokaa madarakani muda mrefu.

“Asili ya Mbeya ni wapinzani sasa kwanini jiji la Mbeya ni chafu ni kutokana na aina ya viongozi tunaokuwa nao, walikuwepo CHADEMA walifanya kwa sehemu yao sasa wamekuja CCM lakini hamna wanachokifanya pamoja na kwamba tuna spika wanasema ni Mbunge wa IPU (Rais wa Mabunge Duniani) mimi sioni faida ya IPU kulingana na mazingira yalivyo, Mbeya ni chafu pamoja na kwamba tuna spika, jimbo halieleweki, sasa ni zamu yetu (wapinzani) kwenda kuibadilisha Mbeya yetu”, amesema Ibrahim.

Amesema ikiwa wapinzani wataungana itakuwa rahisi kushinda uchaguzi mkuu wa 2025 na kwenda kukemea na kuzuia maovu mbalimbali nchini ikiwemo utekaji, mauaji, uminyaji haki za wananchi na kuleta maendeleo ya kweli akidai Chama Cha Mapinduzi na viongozi wake hawana dhamira ya kweli kuwaletea maendeleo wananchi.

Alipoulizwa kinachoendelea ndani ya CHADEMA ikiwa kinachagiza kukua kwa demokrasia na upinzani, Katibu Ibrahim Mwakwama amejibu kwamba;

“Kinachoendelea katika siasa za Tanzania ni kichekesho, huu ni wakati ambao wapinzani mimi nilitegemea tungeungana kwa sababu kuiondoa CCM madarakani, sisi wenyewe kama CUF ni ngumu, lakini vyama vingi vimeweka maslahi yao mbele, ni kwa nini tunagombana? Mimi ukiniuliza leo kwamba Lipumba alistahili kuwepo kwenye uenyekiti ningesema hakustahili, ilitakiwa tuone sura mpya ya mwenyekiti wa CUF; ukiniuliza Mbowe anastahili kugombea uenyekiti nitasema hastahili kwasababu tunahitaji kuona mabadiliko, kwasababu tunavyotaka kwenda kuchukua nchi mabadiliko huwezi kuanzia kwa jirani ni lazima uanzie kwako. Mimi siwezi kufurahia kuhama kwa viongozi wa vyama vya upinzani kuhamia vyama vingine mfano Ibrahim Lipumba amerudi basi tumekubaliana kwenda kujenga chama mahali ambapo kilikuwa kimelegalega, CHADEMA ukiangalia kuna makundi mawili, la Mbowe na la Lissu, mimi ningewashauri CHADEMA kama wananisikiliza huu sio wakati wa kugombana bali tunahitaji kuunganisha umoja wetu kwahiyo mimi sikutarajia kuwaona akina Nkurunzinza hawa wawili (Freeman Mbowe na Ibrahim Lipumba) tungewaona vijana wao waendeleze taasisi hizi”, ameeleza katibu huyo wa CUF mkoa wa Mbeya.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!