Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, ameitaka Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji kwa wakati na kuondoa urasimu usio wa lazima unaosababisha ucheleweshaji wa huduma.
Akizungumza siku ya Jumanne Machi 18, 2025 wakati wa ziara yake katika Mradi wa Maji wa Bangulo uliopo mtaa wa Bangulo Hali ya Hewa katika kata ya Pugu Station wilayani Ilala mkoani Dar es Salaam, Waziri Aweso amewataka wahudumu wa dawati la huduma kwa wateja wa DAWASA kutoka maofisini na kuwafuata wananchi moja kwa moja ili kupunguza mianya ya walaghai na vishoka wanaotumia mwanya wa ucheleweshaji kuwaibia wananchi.
“Maelekezo yangu kwa dawati hili la huduma kwa wateja mtoke ofisini mwende kwa wananchi, mkawafuate wananchi, msipowafuata wananchi wanatokea vishoka (walaghai na wadanganyifu). Mwananchi anatakiwa aunganishiwe maji badala ya kulipa fedha ndogo anaongezewa fedha nyingine, hivyo kujenga urasimu usiokuwa wa lazima,” amesema Waziri Aweso.
Aidha, amewaelekeza DAWASA kuhakikisha kuwa kila mteja anayewasilisha maombi ya kuunganishiwa maji hapaswi kusubiri zaidi ya siku saba kabla ya huduma hiyo kutolewa.
“Niwaombe wateja na nyie mliounganishiwa maji, umeunganishiwa maji na umeomba kuunganishiwa maji isizidi siku 7 lazima uwe umeunganishiwa maji, na hakuna kutoa chochote cha ziada kwamba mpaka upite mlango mwingine ndiyo uunganishiwe maji, wewe toa taarifa,” amesisitiza.
Katika hatua nyingine, Waziri Aweso ametoa maagizo kwa DAWASA kubuni utaratibu wa kuwaunganishia maji wananchi ambao hawana uwezo wa kulipa gharama za mara moja, kwa kuwaletea mpango wa malipo ya mkopo kupitia bili zao. Amesisitiza kuwa viwanda na wananchi wanahitaji maji kwa maendeleo yao, hivyo ni muhimu kuweka utaratibu mzuri wa malipo.
“DAWASA tengenezeni utaratibu mzuri, wadau wapo wa viwanda, mtu ukimuunganishia maji maana yake atalipa, wekeni utaratibu mzuri, mkateni katika bili yake kwamba utalipa muda fulani, utalipa muda fulani ili anufaike na matunda ya Rais Samia Suluhu Hassan,” amesema.
Aidha, amekemea vikali tabia ya baadhi ya watendaji wa mamlaka hiyo kubambikizia wateja bili zisizo halali, akisisitiza kuwa wananchi wanapaswa kulipa gharama halisi ya maji waliyotumia.
“Ni marufuku kumbambikizia mwananchi bili ya maji, ametumia maji ya elfu 10 alipe elfu 10, siyo ametumia maji ya elfu 10 unakuja kumwambia laki na 50 kama kiwanda, hapana,” ameonya.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji Mhandisi Mwajuma Waziri amewaomba wananchi wa Bangula kutunza vyema miundombinu ya maji katika eneo lao na kutoa taarifa watakapoona kuna dalili ya kuvuja kwa maji kutokana na baadhi ya mabomba katika eneo hilo kuwa ya muda mrefu. Amesema kwa kufanya hivyo, upotevu wa maji utadhibitiwa na huduma kwa wananchi itaendelea kutolewa kwa ufanisi.
Kwa upande wake Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA Mhandisi Mkama amesema mradi huo umegharimu jumla ya fedha za Kitanzania Shilingu bilioni 36.8 hii inajumuisha gharama ya ujenzi pamoja na usimamizi wa mradi ambapo kwa ujenzi pekee gharama ni Shilingi bilioni 35.0 na usimamizi wa mradi gharama ni Shilingi bilioni 1.8
Amesema kuwa Dar es Salaam upande wa Kusini kulikuwa na changamoto ya maji kutokana na miundo ya kijiografia ya milima lakini kwa mradi huu, wananchi hawatapata shida tena kwani tayari kuna mitandao ya zamani ya maji katika eneo hilo ambayo inaendelea kuboreshwa na kutawekwa mtandao mpya.
Mradi huu unahusisha Manispaa za Ubungo, Temeke, na Jiji la Ilala, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali kuboresha huduma ya maji katika maeneo yenye changamoto ya upatikanaji wa maji ukilenga kunufaisha wananchi 450,000 wa kata wilayani Ilala za Mzinga, Kipunguni, Kitunda, Pugu station na Kiluvya huku kata za Msigani wilayani Ubungo na Kinyerezi wilayani Ilala zikienda kuongezewa msukumo wa maji.
Waziri Aweso ametoa pongezi kwa DAWASA kwa hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa mradi huo, akisisitiza umuhimu wa kuhakikisha huduma zinawafikia wananchi kwa wakati na kwa uadilifu.