Mkuu wa Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam Edward Mpogolo, amewataka viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na serikali kuhakikisha wanakuwa na mahusiano mazuri ili kuhakikisha utekelezaji mzuri wa miradi ya maendeleo.
Akizungumza katika ziara yake kwenye kata za Liwiti, Tabata, na Kimanga, Mpogolo amesema kuwa mahusiano kati ya viongozi wa chama na serikali ni muhimu katika kufanikisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi. Amesema kuwa hata katiba ya nchi inatambua umuhimu wa mfumo wa chama chenye dhamana na serikali iliyopo madarakani, hivyo ushirikiano usio na mipaka ni msingi wa utekelezaji mzuri wa ilani ya uchaguzi na maendeleo ya taifa kwa ujumla.
Kuhusu maandalizi ya uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27, mwaka huu, Mpogolo amewataka wananchi kujiandikisha kwa wakati katika daftari la makazi linalotarajiwa kufunguliwa kuanzia Oktoba 11 hadi 20 mwaka huu.
Amesisitiza kuwa ni muhimu kwa wananchi kushiriki kikamilifu katika uchaguzi huo, kwani ni fursa ya kuwachagua viongozi watakaosaidia kusukuma mbele maendeleo ya mitaa yao.
Alieleza kuwa, “Viongozi wanapaswa kuhamasisha wananchi katika maeneo yao kushiriki uchaguzi kwa kujiandikisha na kupiga kura ili kudumisha umoja, mshikamano, na upendo.”
Akijibu kero mbalimbali zilizowasilishwa na wananchi katika ziara hiyo, Mpogolo ameahidi kuwa halmashauri itahakikisha inatatua matatizo yanayohusiana na elimu, hasa suala la uzio katika Shule ya Sekondari Liwiti, ambayo inazungukwa na shule mbili za msingi. Amesema tatizo hilo litatatuliwa haraka ili kuhakikisha usalama wa wanafunzi.
Kuhusu changamoto ya Mto Msimbazi, Mpogolo ameeleza kuwa serikali inatambua kero hiyo na tayari imeanza kuchukua hatua za kuondoa tatizo hilo, kwani mto huo umekuwa na tabia ya kuhama maeneo yake, jambo ambalo limeleta athari kwa wananchi.
Aidha, Mpogolo amezungumzia tatizo la miundombinu ya barabara katika kata za Tabata, Liwiti, na Kimanga, ambapo ameeleza kuwa baadhi ya barabara ziko kwenye mpango wa matengenezo kupitia mradi wa Mradi wa uendelezaji wa Jiji la Dar es salaam (DMPD), huku nyingine zikishughulikiwa na Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA).
Mpogolo ametoa wito kwa viongozi, wazazi, na walezi kuhakikisha wanasimamia maadili ya watoto, hasa wale waliomaliza darasa la saba, ili kuepuka mimba za utotoni na magonjwa ya zinaa. Amesisitiza kuwa wazazi wana jukumu kubwa la kuhakikisha watoto wanakuwa na malezi bora na wanapata maadili mazuri ili kuepuka changamoto za kiafya na kijamii.