Mkuu wa Wilaya ya Kibaha mkoani Pwani, Nickson Simon ameipongeza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kwa kutoa huduma bora kwa wananchi wa wilaya yake sambamba na kuchochea uwekezaji unaotokana na uwepo wa maji ya uhakika kutoka DAWASA.
Kauli hiyo ameitoa Machi 14, 2025 wakati akifungua Kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa DAWASA kinachofanyika katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere iliyopo Kibaha.
Nickson amesema uhalali wa serikali kuendelea kuwepo ni wananchi kupata huduma za msingi, hivyo DAWASA wanalo jukumu kubwa la kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya majisafi na majitaka ili serikali iendelee kuwepo.

Amesema maji yanaweza kuleta amani au yanaweza kuleta machafuko, hivyo maji ni muhimu, na wanachotaka wananchi wakiomba kuunganishiwa maji, waunganishiwe kwa haraka na maji yatoke kwenye bomba.
“Wawekezaji wakija Pwani sisi tunawaambia tuna uhakika wa maji na hiyo inaongeza uwekezaji katika sekta ya viwanda katika mkoa wetu, sisi kufanya vizuri mkoa wa Pwani kunatokana na uwepo wa maji ya kutosha kutoka DAWASA.” Amesema Nickson.
Mkuu huyo wa wilaya ameitaka DAWASA kuongeza kasi na juhudi katika kutoa huduma kwa wananchi ili kufikia malengo yao na kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora wakati wote.
Kaimu Mtendaji Mkuu DAWASA, Mhandisi Mkama Bwire amesema kuwa vyanzo vyote vya maji yanayotumiwa mkoa wa Dar es Salaam na Pwani asilimia kubwa ya vyanzo hivyo vipo mkoani Pwani.

“Ukiangalia mtambo wa Ruvu Juu, upo Mlandizi, Mtambo wa Ruvu chini upo Bagamoyo, Mtambo wa Wami upo Chalinze kwa ujumla vyanzo hivyo vinatoa asilimia 91 tunayoyazalisha kasoro asilimia 8 tunategemea vyanzo vya visima katika maeneo ya Kigamboni na Mtambo wa Mtoni uliopo Temeke,” amesema.
Mhandisi Bwire, amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kufanikisha utekelezaji wa miradi ya majisafi yenye thamani ya Shilingi trilioni 1.19 kwa kipindi cha miaka 4 ya uongozi wake.
Amesema kuwa kati ya miradi hiyo, Shilingi bilioni 796.19 ni miradi ya majisafi na miradi yenye thamani ya Shilingi bilioni 400.91 ni miradi ya usafi wa mazingira.
Amesema kuwa kati ya miradi hiyo, miradi iliyokamilika ina jumla ya thamani ya bilioni 344.67, ambapo, kati ya hiyo miradi ya majisafi ni Tsh. bilioni 329.97 na miradi ya miradi ya usafi wa mazingira ni Shilingi bilioni 14.7.
Mhandisi Bwire amesema miradi ya majisafi inayoendelea kutekelezwa katika hatua mbalimbali, ambayo ina thamani ya Shilingi bilioni 852.43, ambapo miradi ya majisafi ina thamani ya bilioni 466.22 na miradi ya usafi wa mazingira ina thamani ya Shilingi bilioni 386.21.
Mhandisi Bwire amesema kuwa idadi ya maunganisho ya wateja wa majisafi imeongezeka kutoka 343,019 hadi kufikia wateja 455,720 sawa na ongezeko la wateja 112,701.