Latest Posts

DC MAKILAGI AKERWA VIKUNDI HEWA MIKOPO YA ASILIMIA 10 

 

ANANIA KAJUNI

 

Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi ameonyesha kukasilishwa na kitendo cha baadhi ya vikundi hewa vya vijana, wanawake na wenye ulemavu kuundwa ili kujipatia mkopo wa asilimia 10 inayotolewa kwenye Halmashauri.

 

Akizungumza kwenye hafla ya kukabidhi hundi ya Shilingi Bilioni 1.3 kwenye vikundi 85 vya wanawake, vijana na wenye ulemavu vilivyobahatika kupata mkopo wa asilimia 10 wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza.

 

Makilagi amedai isingekuwa ni umakini uliofanywa na Kamati ya Wilaya kufuatilia kwa undani vikundi hivyo fedha za mikopo hiyo zilikuwa zinaenda kutua mikononi mwa watu wenye nia mbaya.

 

“Kama kamati hii isinge ingia kwa undani tulikuwa tunarudia makosa yale yale, baada ya kamati kuzama nilikuwa nawafuatilia usiku na mchana tulibaini baadhi ya vikundi havikuwa vikundi wengine waliingia kwa nia ovu wapewe ili wakimbie na fedha zetu kama ambavyo tunawadai zaidi ya Bilioni 3,” amesema Makilagi

 

Kutokana na hilo Makilagi amemwagiza Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza na Kamati za Mitaa, Kata na Wilaya kutimiza wajibu wao huku pia Mkurugenzi akitakiwa kuandaa mafunzo ya kuwajengea uwezo kamati hizo.

 

“Nitoe maelekezo kwa Mkurugenzi kuna Bilioni 2.5, nizitaka kamati za mitaa na kata za wilaya zilizopewa jukumu la kufuatilia vikundi hivi kutimiza wajibu wao maana kama wangetimiza wajibu wao hivyo vikundi hewa ambavyo vilikuwa vinaenda kutupelekea kupoteza fedha visingetokea,” amesema.

 

“Lakini pia natoa maelekezo kwa Mkurugenzi, kwenye kamati ya usalama ya wilaya tayari nilishatoa maelekezo mara baada ya shughuli hii kazi itakayofuata tena ni mafunzo kati ya hizi kamati za wilaya na kata wakae na kamati ya usalama iliyohakiki miradi hii ili wahakiki neno kwa neno kwa kile walichokiona ili siku moja majina yetu sisi viongozi yaje yaandikwe kwa wino wa dhahabu,” amesema Makilagi

 

Akizungumzia mikopo hiyo amesema fedha zingine zaidi ya Bilioni 2.5 tayari zipo tayari kukopeshwa kwa wanawake, vijana na wenye ulemavu huku akidai tangu wapokee maelekezo kutoka kwa Rais ya kutenga asilimia 10 mpaka sasa takribani Bilioni 3.8 zimetengwa katika Halmashauri ya Jiji la Mwanza.

 

“Kila fedha inayokusanywa ya Halmashauri asilimia 70 kwa mujibu wa maelekezo inatakiwa iende kwenye miradi ya maendeleo na katika miradi ya maendeleo asilimia 10 inatakiwa iende kwenye mfuko wa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu tangu Rais ameelekeza mpaka sasa ninavyozungumza wameshatenga Bilioni 3.8,” amesema.

 

Kwa upande wake Mbunge Jimbo la Nyamagana, Stanislaus Mabula amewataka watu na vikundi ambavyo bado havijanufaika na mkopo huo awamu ya kwanza kuendelea kufuata taratibu za kuomba mkopo huo huku akidai zaidi ya Bilioni 5 zinakusudiwa kutolewa katika mwaka huu.

 

“Nitoe wito kwa yule ambaye hajapata sasa fedha bado zipo nyingi tunawakaribisha wazingatie masharti lakini pia nitoe wito kwa maafisa maendeleo watu wengi wamekosa ufahamu, elimu na taarifa watumie fursa hii kuwatangazia wananchi kuwaambia zoezi limeshaanza,” amesema Mabula

 

Mmoja ya wanufaika wa mkopo huo ambaye pia ni Katibu wa Umoja wa Madereva Bajaji Buzuruga – National, Ndaki Shigella ameipongeza Serikali kwa kupata mkopo wa milioni 15 wa ununuzi wa bajaji huku akiahidi kurejesha kwa wakati ili kuwanufaisha watu wengine wengi.

 

“Mkopo wa awamu ya kwanza nimenufaika ni Milioni 15 ambapo nimepata bajaji hizi kwa ajili ya kwenda kuanza kazi na kuanza kurejesha marejesho huku matamanio yangu ni kuchukua mkopo awamu ya pili pindi nikifanyakazi kwa uaminifu na kurejesha kwa wakati,” amesema Shigella

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!