Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sixtus Mapunda, amepongeza kuanzishwa kwa jukwaa la Temeke Women’s Gala akieleza kuwa ni hatua muhimu katika kuwawezesha wanawake kiuchumi, kijamii na kimahusiano, huku akisisitiza umuhimu wa mwanamke kuwa mhimili wa maendeleo ya familia na taifa.
Akizungumza katika tukio hilo lililofanyika leo tarehe 31-03-2026 katika Hoteli ya Gate Way, Kijichi jijini Dar es Salaam, Mapunda amesema jukwaa hilo linabeba nguzo tatu muhimu ambazo ni uwezeshaji wa kiuchumi kwa mwanamke, malezi na mahusiano pamoja na kujitambua.

Ameeleza kuwa mahusiano ni dhana pana inayohitaji kuangaliwa kwa kina kwani ina athari kubwa katika ustawi wa familia na jamii, akiongeza kuwa changamoto nyingi zinazowakabili wanawake zinaanzia katika eneo hilo.
“Tunapozungumzia uwezeshaji wa mwanamke kiuchumi, tunazungumzia pia uwezo wake wa kufikiri, kulea na kujenga taifa bora. Mama mwenye uhakika wa mahitaji yake huzaa na kulea watoto katika mazingira bora,” amesema Mapunda.
Kwa upande wake, Mwanzilishi wa Temeke Women’s Gala, Halima Mhando, amesema kuwa jukwaa hilo limeanzishwa kama harakati mpya ya kijamii, kiuchumi na kimkakati inayolenga kumwezesha mwanamke kuwa mhimili wa maendeleo kuanzia ngazi ya familia hadi taifa.

Amefafanua kuwa kupitia jukwaa hilo, wanawake zaidi ya 2,500 kutoka kata zote za Wilaya ya Temeke wanatarajiwa kushiriki, sambamba na wadau mbalimbali wakiwemo wajasiriamali, taasisi za fedha, wawekezaji na makampuni binafsi kwa lengo la kujenga mtandao imara wa kibiashara.
“Temeke Women’s Gala si tukio la siku moja, bali ni mwanzo wa mpango endelevu utakaohusisha kuanzishwa kwa makundi ya wanawake katika kila kata, yatakayosaidia uratibu wa shughuli, uwezeshaji wa kiuchumi na upatikanaji wa fursa za mitaji na masoko,” amesema Mhando.
Aidha, ameangaza kuwa msimu wa kwanza wa gala hilo unatarajiwa kufanyika Mei 31 katika viwanja vya Sabasaba, ambapo pamoja na shughuli za kujifunza na kuunganisha wanawake, kutakuwa na utoaji wa tuzo maalum kwa wanawake waliofanya vizuri katika sekta mbalimbali ikiwemo biashara, uongozi, ubunifu, teknolojia na huduma kwa jamii.
Aliongeza kuwa tiketi za kushiriki zitapatikana katika vituo mbalimbali pamoja na mitandao ya kijamii, ambapo tiketi za kawaida zitauzwa kwa shilingi 30,000, VIP shilingi 50,000 na daraja la juu zaidi shilingi 70,000, huku meza ya watu 10 ya VIP ikiuzwa kwa shilingi 700,000.
