Na Josea Sinkala, Mbeya.
Mkuu wa wilaya ya Mbeya Mhe. Beno Malisa, amefanya ziara katika kata ya Utengule Usongwe kwa lengo la kukagua hali ya uripoti wa wanafunzi waliofaulu kwa ajili ya kuanza kidato cha kwanza kwa shule za sekondari mwaka 2025.
Ziara hiyo ameifanya jumanne hii (Februari 11, 2025) ambapo akitoa taarifa kwenye eneo la elimu ya sekondari, Kaimu mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Mbeya ambaye pia ni afisa elimu sekondari Mwalimu Aliko Mbuba amesema hadi sasa jumla ya asilimia 81 ya wanafunzi wanaotakiwa kuripoti shuleni kwa eneo la sekondari wameshaanza masomo na kwa ambao bado idara ya elimu inaendelea kushughulikia ili kuhakikisha wazazi na walezi wanawajibika kuwapeleka hata wasipokuwa na vifaa vya shule ikiwemo sare.
Akitoa maelekezo ya Serikali baada ya kutembelea shule za sekondari Ihombe na Juhudi Usongwe, mkuu wa wilaya ya Mbeya Mhe. Beno Morris Malisa, ameelekeza kupata taarifa za maendeleo ya uhamasishaji watoto kuripoti shuleni kila junanne hadi mwishoni mwa mwezi Februari 2025 huku pia akiagiza wazazi na walezi watakaoshindwa kuwajibika basi wawajibushwe wao kwasababu Serikali imeweka mazingira rafiki kuhakikisha watoto wanapata haki yao ya msingi ya elimu.
Mkuu wa Polisi wilaya ya kipolisi Mbalizi SSP Mathew Mgema, amesema Polisi wilayani Mbalizi itahakikidha inashirikiana na watendaji wa kata na askari kata kuwachukulia hatua wazazi na walezi watakaoshindwa kuwapeleka shule watoto wao kuanza masomo hasa ya sekondari.
SSP Mgema ametumia fursa hiyo kuwataka wananchi kuhakikisha wanawapeleka watoto shuleni kabla ya kufikiwa na mkono wa dola kwani elimu ni kwa faida yao na Taifa kwa ujumla.
Maafisa elimu kata za Iwindi, Utengule Usongwe na Nsalala wameahidi kuhakikisha wanaendelea kuhimiza watoto kutambua umuhimu wa elimu na wazazi na walezi kuhakikisha wanawapeleka watoto wao shuleni kuanza masomo ya sekondari na kuchukua hatua kwa watakaoshindwa kuwapeleka shule watoto wao.