Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, amewataka Watanzania kuendelea kuthamini na kulinda mchango wa wazee katika jamii. Akizungumza na kituoc ha habari cha Uhuru FM kuhusu Siku ya Wazee Duniani, inayoadhimishwa duniani kila mwaka Oktoba 1, Mpogolo amesema ni muhimu kwa jamii kutambua mchango wa wazee katika maendeleo ya taifa, mikoa, na wilaya.
Amesisitiza kuwa jukumu la kuwatunza wazee linapaswa kuanzia kwenye familia kwa kuhakikisha wanapata heshima na nafasi ya kutoa mawazo, busara, na hekima zao. Mpogolo amekemea tabia ya kuwatenga wazee au kuwapeleka kwenye makazi ya wazee wakati familia bado ipo na inawajibika kuwaweka karibu.
Amesisitiza zaidi kuwa wazazi wana jukumu la kuwafundisha watoto wao kuhusu maadili ya kuwaheshimu wazee, hususan katika maeneo ya umma kama kwenye vyombo vya usafiri, ambako wazee wanapaswa kupishwa nafasi.