Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, ameshiriki zoezi la kujiandikisha katika maboresho ya Daftari la Kudumu la Mpiga Kura katika Kata ya Ilala, Mtaa wa Karume, jijini Dar es Salaam.
Mpogolo alifika katika kituo cha kuandikisha wapiga kura leo asubuhi na kuungana na wananchi waliokuwa wakisubiri kuboresha taarifa zao. Akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Ilala, amewahimiza kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika vituo vyao ili kushiriki kikamilifu katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
“Zoezi hili la wiki moja ni muhimu kwa kila mwenye sifa ya kupiga kura. Ni fursa kwa kila mmoja kujiandikisha au kuboresha taarifa zake, hasa kwa waliobadili maeneo ya makazi. Hatua hii itahakikisha kila mwananchi anapata haki yake ya msingi ya kupiga kura kwa ajili ya kuchagua viongozi wetu,” amesema Mpogolo.
Amesisitiza kuwa ushirikiano kutoka kwa wenyeviti wa serikali za mitaa na wajumbe wao ni muhimu katika kuwahamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi ili zoezi hili lifanikiwe.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Karume, Hajji Bechina, amesema zoezi hilo limekuwa na mwitikio mzuri tangu kuzinduliwa Machi 17, 2025, huku wananchi wakiendelea kujitokeza kwa wingi.
Maboresho ya Daftari la Kudumu la Mpiga Kura katika Mkoa wa Dar es Salaam yanatarajiwa kukamilika Machi 23, 2025, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge, na Madiwani unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwaka huu.