Latest Posts

DC MPOGOLO: MUUNGANO NI TUNU, KILA MTANZANIA ANA DHAMANA YA KUULINDA

Wananchi wa Wilaya ya Ilala, jijini Dar es Salaam, wameungana na Watanzania wengine kote nchini kuadhimisha miaka 61 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, kwa kushiriki shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo usafi wa mazingira, upandaji miti na usafishaji wa fukwe za Bahari ya Hindi.

Katika hotuba yake kwa wananchi, viongozi na wadau waliokusanyika katika Soko la Samaki Fely, Mkuu wa Wilaya ya Ilala Edward Mpogolo amesisitiza kuwa Muungano ni dhamana ya kila Mtanzania na kila mmoja anapaswa kuutunza, kuuenzi na kuutetea kwa vitendo.

“Muungano wa miaka 61 uliasisiwa kwa hekima na busara na waasisi wetu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Shekhe Abed Amani Karume. Tunapaswa kuuenzi kama tunu ya Taifa,” amesema Mpogolo.

Mpogolo ameeleza kuwa Soko la Samaki Fely ni mfano hai wa matunda ya Muungano, likiwa ni mahali ambapo Watanzania wa makabila na tabaka mbalimbali kutoka bara na visiwani wanakutana, kufanya biashara na kuishi kwa mshikamano.

Akieleza kuhusu kaulimbiu ya mwaka huu, “Muungano Wetu ni Dhamana, Heshima na Tunu ya Taifa: Shiriki Uchaguzi Mkuu wa 2025”, Mpogolo amewahimiza wananchi kushiriki kikamilifu katika uchaguzi mkuu kwa kuchagua viongozi bora watakaoendeleza tunu ya Muungano na kulinda amani ya nchi.

“Kila Mtanzania ana jukumu la kushiriki uchaguzi na kuchagua viongozi wanaoenzi Muungano huu wa kihistoria,” ameongeza.

Mkuu huyo wa Wilaya alieleza kuwa licha ya Ilala kuwa na idadi kubwa ya watu — zaidi ya milioni tatu wakati wa mchana na zaidi ya milioni moja usiku — bado inaendelea kuwa na hali ya amani, umoja na mshikamano, hali ambayo ni matokeo ya kudumishwa kwa Tunu za Muungano.

Mpogolo amelipongeza Jeshi la Uhamiaji kwa ushirikiano katika kuhakikisha wageni wanaoingia Ilala kwa njia za anga, reli na maji wanatii sheria na taratibu za nchi, jambo linalosaidia kuimarisha usalama na mshikamano wa kitaifa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Jiji la Ilala Elihuruma Mabelya amewasihi vijana kuwa na uzalendo wa dhati kwa kutunza na kuendeleza Muungano.

Naye Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Omary Kumbilamoto, amesisitiza kuwa Muungano umejenga udugu, ujamaa na kusaidia kuondoa kero za kiutawala zilizokuwepo miaka ya nyuma baina ya bara na visiwani.

 

Katika kilele cha maadhimisho hayo, wananchi wa Ilala wametumia fursa hiyo kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa juhudi zao katika kulinda na kuimarisha Muungano, sambamba na kuleta maendeleo katika sekta mbalimbali za nchi.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!