Mkuu wa Wilaya ya Arusha Felician Mtahengerwa amemshukuru Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kurejesha tena fedha za mikopo kwa wanawake, vijana na wenye ulemavu ikiwa ni jitihada zake za kuinua uchumi wa mwananchi mmojammoja.
Mtahengerwa ametoa kauli hiyo Ijumaa Septemba 06, 2024 kwenye viwanja vya Kilombero wakati wa uzinduzi wa utoaji mikopo kwenye Halmashauri ya wilaya ya Arusha ambapo Shilingi bilioni 6 na milioni 233 zitatolewa kwa makundi hayo.
“Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi mahiri wa Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kutekeleza azma yake ya kutoa huduma bora na kuboresha maisha ya Watanzania. Katika kuboresha hali zao za kiuchumi serikali inatekeleza kwa vitendo azma ya kukuza uchumi na kuongeza ajira kwa wananchi kwa kuwakopesha mitaji wafanyabiashara wadogo na wa kati ili waweze kujiinua kiuchumi”, amesema Mtahengerwa.
Katika hatua nyingine Mtahengerwa ametumia sehemu ya hotuba yake kuwaomba wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa kwa kugombea na kuchagua viongozi wa Vijiji, mitaa na vitongoji katika kujiletea maendeleo.