Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Felician Mtahengerwa, amemshukuru Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa kuonesha kujali makundi maalumu ya vijana, wanawake, na watu wenye ulemavu, kupitia utoaji wa mikopo ya Shilingi za Kitanzania bilioni 6.3.
Mtahengerwa ametoa kauli hiyo Septemba 05, 2024 wakati akitangaza uzinduzi rasmi wa msimu wa utoaji wa mikopo hiyo, zoezi ambalo linafanyika Ijumaa hii ya Septemba 06, 2024 kwenye viwanja vya Kilombero.
Mtahengerwa amewaambia wanahabari kuwa katika uzinduzi huo, elimu na ujuzi mbalimbali utatolewa kwa wahudhuriaji ikiwa ni mwanzo wa kuwaandaa vijana, wanawake na wenye ulemavu kuweza kuingia kwenye mchakato wa kuwa wanufaika wa fedha hizo za mkopo.