Latest Posts

DC RUFIJI ALA KIAPO, RC KUNENGE ATOA MAAGIZO

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge amewataka Wakuu wa Wilaya mkoani humo kushirikiana kikamilifu katika utendaji kazi kulingana na uwezo wao, huku wakifanya maamuzi sahihi ambayo yatasaidia kuchochea maendeleo katika wilaya zao.

Maelekezo haya yametolewa mnamo Septemba 5, 2024 wakati wa hafla ya kuapishwa kwa Mkuu mpya wa Wilaya ya Rufiji, Luteni Kanali Fredrick Komba aliyechaguliwa hivi karibuni na Rais Samia Suluhu Hassan.

Kunenge amesisitiza kuwa ushirikiano kati ya wakuu wa wilaya na uongozi wa mkoa ni muhimu katika kuhakikisha malengo ya maendeleo yanatimizwa ipasavyo.

Katika hotuba yake, Kunenge amewakumbusha wakuu wa wilaya umuhimu wa kusimamia masuala ya ulinzi na usalama katika maeneo yao, akisema kuwa jukumu hilo ni msingi wa ustawi wa maendeleo.

Aidha Kunenge aliwataka kuendelea kusimamia utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), huku wakijenga uhusiano mzuri na chama hicho. Ameeleza kuwa ni muhimu viongozi kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu na kuepuka urasimu ambao unaweza kukwamisha juhudi za serikali za kufanya mapinduzi ya viwanda mkoani Pwani.

Kwa upande wake Luteni Kanali Fredrick Komba ameahidi kufanya kazi kwa mujibu wa kiapo chake na kuhakikisha anatekeleza maono ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa maslahi mapana ya wananchi wa Wilaya ya Rufiji. Komba ameahidi kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuhakikisha wilaya yake inapata maendeleo endelevu.

Mkoa wa Pwani una wilaya saba, ambapo katika mabadiliko yaliyofanywa na Rais Samia hivi karibuni, Wilaya za Bagamoyo na Rufiji ndizo zilizopata Wakuu wapya wa wilaya. Shaibu Ndemanga amehamishiwa Wilaya ya Bagamoyo, huku Luteni Kanali Fredrick Komba akiteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Rufiji.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!