Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Mkoani Mara, Kemilembe Lwota, ameonya vikali wote wanaojihusisha na vitendo vya ukatili wa kijinsia katika wilaya hiyo, akisisitiza kuwa hakuna atakayeponea endapo atabainika kuhusika.
Katika hotuba yake aliyotoa alipokuwa akitembelea Kituo cha Hope for Girls and Women Tanzania kilichopo Mugumu, Kemilembe Lwota amesema serikali imejipanga kuchukua hatua kali dhidi ya wahusika wa vitendo vya ukeketaji, ulawiti, ubakaji, na vipigo kwa wanawake na watoto.
“Tumeazimia kwa dhati kuhakikisha kuwa watoto na wanawake wanakuwa salama. Hakuna atakayeponea endapo atabainika kuhusika na vitendo hivi vya kikatili,” amesema Lwota.
Ametoa wito kwa wananchi wa Serengeti kutofumbia macho vitendo hivyo na kutoa taarifa mara moja wanapobaini visa vya ukatili wa kijinsia.
“Niwaombe sana wakazi wa Serengeti, msifiche wala kufumbia macho vitendo hivi. Wengine wanavifanya ndani ya jamii yetu, hivyo ni jukumu letu sote kuhakikisha tunavitokomeza,” amesisitiza Mkuu wa Wilaya.
Katika hatua nyingine, Lwota ameagiza maafisa wa serikali wanaohusika na udhibiti wa vitendo vya ukatili wa kijinsia kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao ipasavyo, ikiwemo kutoa elimu kwa wananchi katika maeneo yote yaliyoathirika na vitendo hivi.
“Tunahitaji juhudi za pamoja. Maafisa wa serikali hawapaswi kulegalega. Wajibu wao ni kuhakikisha elimu inawafikia watu wote ili kukomesha kabisa vitendo hivi,” ameongeza.
Serikali ya Wilaya ya Serengeti imejipanga kuhakikisha kuwa inawalinda watoto na wanawake dhidi ya ukatili wa kijinsia kupitia mikakati mbalimbali, ikiwemo kuimarisha usimamizi wa sheria dhidi ya wahusika wa ukatili, kutoa elimu ya athari za ukatili wa kijinsia kwa jamii, kushirikiana na taasisi za haki za binadamu kama vile Hope for Girls and Women Tanzania katika kuzuia vitendo vya ukatili.