Na Josea Sinkala; Mkwajuni, Songwe.
Mkuu wa Wilaya ya Songwe mkoani Songwe Solomon Itunda, amezindua mgodi wa madini wenye mtambo mkubwa wa kuchenjua dhahabu ili kuziongozea thamani, mradi uliogharimu shilingi bilioni nane hadi sasa.
Mkuu wa wilaya ya Songwe, akizungumza na mamia ya wananchi na watumishi mbalimbali wa Serikali na sekta binafsi kwenye shughuli ya kuzindua mgodi huo, amesema mwekezaji wa mgodi huo kwa ajili ya kuchakata/kuchenjua dhahabu amejitahidi ili kuinua uchumi na kuwataka wananchi kufanya kazi kwa bidii badala ya kuamini imani za kishirikina kuwa wanaofanikiwa ni freemason.
Itunda amesema Serikali itaendelea kuboresha miundombinu ya wawekezaji ikiwemo kuimarisha nishati ya umeme, barabara na huduma ya maji kwa wananchi wake na kumpongeza mwekezaji huyo ambaye atatoa ajira miambili baada ya uimarishaji mradi huo ambao umefunguliwa.

Akitoa taarifa ya kampuni hiyo, Katibu na mwanasheria wa kampuni ya Green pacific investment limited Dauson David Lugenya, amesema mwekezaji alianza kama mchimbaji binafsi mwaka 2011 hadi kufikia sasa ambapo ameanzisha kampuni (taasisi) na amesema kuzinduliwa kwa kiwanda hicho kutaongeza thamani na ubora wa madini na kuyafanya kuwa na ubora wa juu ndani na nje ya nchi.
Katibu huyo amesema mradi huo utatoa nafasi za ajira kwa jamii kuanzia inayozunguka mradi huo.
“Lengo la mradi na kiwanda hiki ni kuongeza thamani ya madini ya dhahabu kwa kutumia teknolojia ya kisasa ili kufikia kiwango cha juu cha uzalishaji na ubora wa bidhaa (dhahabu). Mtambo wa CIP with floatation machine itaboresha mchakato wa uchenjuaji dhahabu kwa kuchanganya mbinu za kisasa za uchimbaji, uchenjuaji na urejeshaji wa madini yenye viwango vya juu”, amesema mwanasheria na Katibu huyo wa kampuni.
Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Songwe CPA Cesilia Kavishe, amempongeza mwekezaji huyo kwa kuziishi ndoto zake na kuwa msaada kwa jamii kushiriki shughuli za kimaendeleo kwa fedha zake.

Pia Kavishe amewataka wananchi kuchangamkia fursa ya mikopo ya asilimia kumi ya Halmashauri ili kuwekeza.
Kaimu afisa madini mkoa wa Songwe Richard Seyaza, pamoja na kumpongeza mwekezaji huyo amemtaka kuhakikisha anahifadhi mazingira na kufuata taratibu na sheria za uchimbaji na uchenjuaji madini.
Mbunge wa jimbo la Songwe mwalimu Philip Mulugo, ameshukuru uthubutu wa mwekezaji huyo ambaye amemtaja kama mfano wa kuigwa kwani alianzia chini hadi kufikia hatua ya kumiliki mtambo mkubwa wa kuchenjua dhahabu kisasa, mtambo ambao umegharimu shilingi billion nane na hadi kukamilika kwake utagharimu shilingi billion ishirini.
Samweli Lusekelo Ndagile, Afisa Mtendaji kata ya Mbangala, anasema uwepo wa mgodi huo ni fursa kwa wananchi wake wa kitongoji cha Mbangala B. kata ya Mbangala na Halmashauri kwa ujumla.
Mkurugenzi wa kampuni ya Green pacific investment Fredrick Ashely Meshack amewashukuru viongozi na wananchi kwa ushirikiano wao na kuwaasa kuwa na nidhamu, kufanya kazi kwa bidii ili kufikia ndoto zao badala ya kuendekeza maisha ya anasa.
Mtambo wa kuchenjulia madini wa CIP una uwezo wa kuchakata tani kumi za dhahabu kwa saa moja kutoka tani tatu kwa saa moja hivyo itaongeza uzalishaji kwa mwekezaji huyu katika kukuza uchumi wake na Serikali kwa ujumla.
Kampuni ya Green pacific investment (company) limited yenye makao yake makuu jijini Arusha inafanya shughuli mbalimbali ikiwemo shughuli za uchimbaji madini zilizowekezwa katika wilaya na mkoa wa Songwe.