Mkuu wa Wilaya ya Tabora, mkoani Tabora, Bi. Upendo Wella, amewataka wazazi na walezi wilayani humo kuacha mara moja tabia ya kuwaficha watoto majumbani badala ya kuwapeleka shule, ili kuwatumikisha katika shughuli za mashamba ya Tumbaku.
Bi. Wella amesisitiza kuwa mzazi au mlezi yeyote atakayebainika kufanya vitendo hivyo atachukuliwa hatua kali za kisheria kwa mujibu wa sheria za nchi, akieleza kuwa elimu ni haki ya msingi ya kila mtoto.

Wito huo umetolewa mara baada ya kukamilika kwa zoezi la upandaji wa miti ya kivuli na mbao zaidi ya 300 katika Shule ya Msingi Hengele pamoja na shamba la miti la Chama cha Msingi cha Itonjanda, kilichopo Kata ya Itonjanda, Manispaa ya Tabora. Zoezi hilo lililoratibiwa na Bodi ya Tumbaku Mkoa wa Tabora ambapo ni mikakati ya utunzaji wa mazingira na pia ni sehemu ya maadhimisho ya kumbukizi ya siku ya kuzaliwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa Bodi ya Tumbaku Kanda ya Tabora, Bw. Sosthenes Kikwelele, amesema kuwa lengo la upandaji miti ni kuunga mkono juhudi za Serikali katika kutunza mazingira pamoja na kutekeleza masharti ya mikataba ya kimataifa ya ununuzi wa zao la tumbaku.
Naye Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Tabora, Bw. Venance Msafiri, amesema zoezi hilo litakuwa endelevu, akibainisha kuwa mbali na faida ya utunzaji wa mazingira, miti ni mhimili mkubwa katika shughuli za ukaushaji wa tumbaku.
Baadhi ya wananchi wanaoishi katika maeneo ambayo miti hiyo imepandwa, akiwemo Dotto Rajabu, wameahidi kuitunza miti hiyo ili kulinda mazingira na kuchangia ongezeko la mvua katika maeneo yao.