Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga, Joseph Kashushura amewapongeza wananchi wa Kata ya Mkako kwa juhudi zao katika kuunga mkono serikali katika kuboresha mazingira ya elimu.
Wananchi hao wametoa eneo la ekari 7 katika Kitongoji cha Muungano, Kijiji cha Lihale, kwa ajili ya kujenga shule shikizi, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kupunguza umbali wanafunzi wanatembea kufuata elimu.
Katika ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo na kusikiliza kero za wananchi, Mkurugenzi Kashushura aliwapongeza kwa kujitolea katika ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa na ofisi moja ya walimu, mradi ambao tayari umefikia hatua ya renta.

“Huu ni utekelezaji wa kimkakati. Madarasa haya yakikamilika yatawasaidia wanafunzi kutotembea umbali mrefu. Naahidi kuongeza nguvu kwa kutoa saruji na nondo ili kuhakikisha mradi huu unakamilika kwa wakati.” Alisema.
Aidha, Mkurugenzi aliahidi kutoa shilingi milioni 5 kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa ofisi ya Kijiji cha Lihale, kuonyesha dhamira yake ya kuunga mkono juhudi za wananchi.
Afisa Elimu wa Kata ya Mkako, France Komba, alieleza kuwa shule hiyo shikizi inatarajiwa kukamilika mapema ili ifikapo Januari 2025 iweze kuwahudumia wanafunzi waliokuwa wakitembea zaidi ya kilometa tano kwenda shule mama.
Kwa jitihada hizi, wananchi wa Mkako wanatarajiwa kupunguza changamoto za umbali kwa wanafunzi, huku serikali ikiendelea kuunga mkono juhudi za wananchi kwa kutoa vifaa na fedha za kukamilisha miradi.