Latest Posts

DED MILLAO AWAONGOZA WANANCHI ZOEZI LA USAFI SHULE MPYA SEKONDARI YA MNENIA

Mapema Januari 22, 2025, Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa, mkoani Dodoma, Shaban Millao, timu ya Wataalam kutoka Halmashauri pamoja na wananchi wa kijiji cha Mnenia Kata ya Mnenia wamejumuika pamoja katika usafi wa mazingira ya Shule Mpya ya Sekondari ya Mnenia.

Katika zoezi hilo Millao amewapongeza wananchi hao kwa ushirikiano mkubwa waliouonesha kwa kipindi chote cha ujenzi wa Sekondari hiyo kwa kuonesha juhudi binafsi za kujenga darasa kwa nguvu za wananchi.

“Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kutambua jitihada zenu za uhitaji wa shule ya Sekondari ilitenga fedha zaidi ya Shilingi milioni 544 ambazo zimetumika kujenga miondombinu ya kisasa kwa watoto wetu kusomea, tuna kila sababu za kuishukuru serikali yetu, jitihada za Mhe. Mbunge wetu Dkt. Ashatu Kijaji pamoja na Diwani mwenyeji Mhe. Abdalah Maguo zimesaidia shule hii kufikia hapa”. Amesema Millao.

Millao amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu bora katika mazingira rafiki ikipunguza umbali mrefu zaidi ya KM 7 kufuata elimu katika Shule ya Sekondari IMBAFI, na kuwataka wazazi kufuatilia maendeleo ya wanafunzi hao.

Kwa upande wake Mhandisi wa Halmashauri Eng. John Chizima amesema shule hiyo imejengwa kwa fedha za Serikali kupitia mfumo wa “Force Account” ambao huwanufaisha wananchi wa mradi ulipo, akipongeza hali ya usalama wa vifaa vilivyotumika kipindi chote cha ujenzi pasipo uharibifu wowote kufanywa na wananchi hao na baadhi yao kuwa miongoni mwa mafundi wanaojenga majengo hayo.

Nao baadhi ya wananchi waliojitokeza shuleni hapo wamemshukuru Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za ujenzi wa shule hiyo mpya ambayo itarahisisha kupunguza umbali mrefu kwa wanafunzi.

Shule mpya ya sekondari Mnenia inatarajiwa kupokea jumla ya wanafunzi 125 wa kidato cha kwanza mwaka huu 2025 pamoja na wanafunzi wasiopungua 60 wa kidato cha pili ambao watahamishwa kutoka shule mama Sekondari ya IMBAFI.

Katika kuzingatia umuhimu wa lishe na utunzaji wa mazingira, jumla ya miti 550 ikijumuisha miti ya matunda 250 na miti zaidi ya 300 ya kivuli imepandwa kuzunguka mazingira ya shule.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!