Latest Posts

DIRA 2050 KUWEZESHA UKUAJI WA VIWANDA ILI KUONDOA UTEGEMEZI KUTOKA NJE

Serikali imesema katika maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 imeweka kipaumbele kikubwa kwenye maendeleo ya viwanda nia ikiwa ni kuondoa utegemezi wa kununua bidhaa nyingi nje ya nchi.

Hayo yamesemwa siku ya Jumanne Julai 23, 2024 jijini Dar es Salaam na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Profesa Kitila Mkumbo wakati akizungumza kwenye mkutano wa wadau wa viwanda ulioandaliwa na Shirikisho la Wenye Viwanda (CTI), ambao pia ulizindua tuzo za Rais za Mzalishaji Bora Viwandani PMAYA ambazo hufanyika kila mwaka kwa wenye viwanda.

Profesa Kitila amesema wasomi mbalimbali wamesema kwenye maandiko yao kuwa tofauti kubwa baina ya nchi tajiri na zile masikini ni kwamba nchi tajiri zina viwanda vingi wakati nchi masikini hazina viwanda na zinategemea kununua bidhaa nje ya nchi.

“Itakuwa vigumu sana kutengeneza Dira ya Taifa bila kuweka viwanda katikati ya dira hiyo kwa sababu hilo ni la msingi na tafiti nyingi zinaonesha kuwa hatuwezi kuendelea kwa kuendelea kununua bidhaa nje ya nchi, lazima tuwe na viwanda vingi tuuze nje,” Amesema Profesa Kitila.

Amesema katika utafiti ambao umefanywa na serikali katika maandalizi ya dira hiyo uliohusisha watu 7,668 nchi nzima waliochaguliwa kisayansi walitaka vipaumbele vitano viwepo kwenye dira hiyo.

Ametaja moja ya vipaumbele vilivyotajwa na wananchi hao ni suala la viwanda na kwamba asilimia 65 ya malighafi zinazotumika viwandani zinatokana na kilimo hivyo kilimo nacho kitaendelea kuwa kipaumbele kwenye dira hiyo.

Amesema kipaumbele kingine kilichotajwa kwenye utafiti huo ni uwekezaji mkubwa kwenye rasilimali watu kwani uchumi wa viwanda unahitaji watu waliosoma vizuri.

“Lazima dira yetu ituelekeze kuwekeza kwenye elimu na siyo elimu tu bali elimu iliyobora,” Amesema Profesa Mkumbo.

Naye Mwenyekiti wa CTI, Leodegar Tenga amesema wadau wa viwanda wamekutana kujadili dira ya 2050 na kuzungumzia maendeleo ya viwanda kwa ujumla ili kuhakikisha maendeleo ya viwanda hayasahauliki kwenye dira hiyo.

“Hakuna nchi duniani hata moja ambayo iliwahi kupiga hatua kubwa kiuchumi bila kuwekeza kwenye viwanda kwa hiyo lazima tuwe na mikakati madhubutu na kuna msemo wa Kiswahili kwamba kupanga ni kuchagua kwa hiyo tuchague kuwekeza kwenye viwanda ili tusonge mbele,” Amesema Tenga.

Amesema ili viwanda viweze kufanya kazi vizuri lazima serikali iwekeze pia kwenye ujenzi wa miundombinu ya barabara na reli na kuwekeza kwenye rasilimali watu.

“Maono ya nchi ni kujipanga ili tutimize tulichopanga kwa hiyo sisi CTI tunaamini viwanda ni muhimu na ili kupata rasilimali lazima tuwe na kilimo kwa hiyo lazima tuwekeze pia kwenye kilimo, tumefungua masoko mengi upande wa Afrika Mashariki (EAC), kusini mwa jangwa la sahara (SADC) sasa tujipange kuuza bidhaa zetu za viwanda nje ya nchi badala ya sisi kuwa soko la bidhaa za wenzetu,” Amesema Tenga.

Makamu Mwenyekiti wa CTI, Paul Makanza amesema nchi inapaswa kuwa na viwezeshaji vinavyofaa kama teknolojia, rasilimali watu na miundombinu.

“Zaidi ya hayo, ni lazima tujenge msingi imara wa amani, utulivu, umoja, kujitegemea, na muundo wa utawala unaounga mkono uwajibikaji, uwazi na kufanya maamuzi shirikishi, lazima tutafakari kuhusu maisha yetu ya zamani, tuelewe maisha yetu ya sasa, na kwa ujasiri kuunda maisha yetu ya baadaye na tunahitaji maono wazi yanayoungwa mkono na chaguzi za kimkakati na inayoungwa mkono na maadili” Amesema Makanza.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!