Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko, amesema kuwa Serikali itaendelea kuvutia wawekezaji katika tafiti na uchimbaji wa mafuta na gesi nchini, ili kuhakikisha Watanzania wananufaika ipasavyo na rasilimali zilizopo.
Akizungumza Septemba 10, 2024, katika hafla ya makabidhiano ya leseni ya uendelezaji wa gesi asilia kati ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na ARA Petroleum katika Kisima cha Ruvuma Ntorya mkoani Mtwara, Dkt. Biteko alisisitiza kuwa hatua hizi ni matunda ya kazi nzuri inayofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
“Yote haya mnayoyaona ni matunda ya kazi nzuri ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan,” alisema Dkt. Biteko.
Aidha, alieleza kuwa jitihada za Serikali zinaenda sambamba na kuliwezesha TPDC kushiriki kikamilifu katika mnyororo mzima wa thamani wa mafuta na gesi. Alitoa wito kwa TPDC na ARA Petroleum kuhakikisha kuwa wanatoa kipaumbele kwa wazawa katika utoaji wa ajira, ili kuhakikisha kuwa wananchi wanashiriki na kufaidika na maendeleo ya kiuchumi kwenye maeneo yenye miradi hiyo.
Dkt. Biteko pia aliwataka Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kuhakikisha umeme unafika katika maeneo yenye miradi ya gesi kama vile Madimba, Msimbati, na Songosongo ifikapo Desemba mwaka huu.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Kirumbe Ng’enda, aliipongeza Serikali kwa kutoa leseni ya uendelezaji wa kitalu cha gesi cha Ruvuma. Aliitaja hatua hiyo kuwa ni kubwa kwa maendeleo ya sekta ya nishati nchini.
“Kitalu hiki kitazalisha futi za ujazo trilioni 1.6, hili ni jambo kubwa sana na la kuipongeza Serikali. Tunampongeza Rais Samia ambaye yeye ndiye jemedari wa mapambano ya kuleta maendeleo nchini,” alisema Mhe. Ng’enda.
Ng’enda pia alieleza kuwa gesi hiyo itatoa mchango mkubwa katika uendeshaji wa mitambo, magari, na upatikanaji wa nishati safi ya kupikia, hasa baada ya kuongezeka kwa umeme wa megawati 705 unaotokana na mradi wa umeme wa Julius Nyerere.
Awali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mha. Felchesmi Mramba, alieleza kuwa Tanzania ina historia ndefu ya matumizi ya gesi asilia tangu kugunduliwa kwa rasilimali hiyo katika visiwa vya Songosongo miaka ya 1970. Aliongeza kuwa ugunduzi huo umefungua njia endelevu ya kuhifadhi mazingira na kuimarisha usalama wa nishati nchini.