Mbunge wa Jimbo la Kisarawe Dkt. Selemani Jafo ambaye pia ni Waziri wa Viwanda na Biashara ameisitiza Wakala wa Maji Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) wilayani Kisarawe mkoani Pwani kuweka mazingira rafiki kwa wananchi wanaotaka kuvuta maji katika nyumba zao.
Dkt. Jafo ametoa rai hiyo akizungumza mara baada ya kuzindua mradi wa maji katika kijiji cha Mtu nani Kata ya Vikumburu wilayani humo akiwa katika ziara ya kuwasilisha utekelezaji wa ilani jimboni pamoja ma kusikiliza na kutatua kero za wwananchi.
Amesema hatua hiyo itawawezesha wananchi kulipa gharama halisi ya maji waliyotumia na kupunguza manung’uniko miongoni mwa wananchi.
Aidha Dkt. Jafo amewasihi wananchi kulinda miundombinu ya miradi hiyo ili iweze kudumu na kumaliza kabisa shida ya upatikanaji wa maji safi na salama karibu na jamii kama ilivyo dhamira ya serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kumtua mama ndoo kichwani.
Katika hatua nyingine, Jafo amesema Rais Samia Suluhu Hassan ameridhia ujenzi wa kilomita 34.5 kwa kiwango cha lami katika Barabara ya Kisarawe kwenda Mloka huku akieleza kusikitishwa na baadhi ya watu wakiwemo viongozi wa Jumuiya za Chama cha Mapinduzi wanaoandika mitandaoni wakibeza hatua hiyo ya Rais Samia kuridhia ujenzi wa kipande hicho cha barabara.