Waziri wa Fedha Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba ameihakikishia Jumuiya ya Kimataifa na Watanzania kwa ujumla kwamba Serikali inaendelea kuweka na kuboresha mazingira ya uwekezaji ikiwamo kuboresha mifumo yake ya kodi.
Dkt. Nchemba ameyasema hayo katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha Jijini Dar es Salaam wakati akiagana na Balozi wa Uswizi aliyemaliza muda wake wa ubalozi nchini Tanzania Didier Chassot.
Amesema kuwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameunda timu ya wataalamu ya kupitia na kuja na mapendekezo yatakayosaidia kuboresha mifumo yake ya kodi ili kuvutia zaidi biashara na uwekezaji nchini.
Dkt. Nchemba amefafanua kuwa pamoja na kuundwa kwa timu hiyo, Serikali pia imechukua hatua kadhaa za kuboresha ya kielektroniki ya ukusanyaji kodi inayosaidia kukusanya mapato yake kwa ufanisi na kuondoa usumbufu kwa walipakodi.
Amesema kuwa lengo la kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji pamoja na kuimarisha mifumo ya kodi ni kuhakikisha kuwa idadi ya walipakodi inaongezeka hatua itakayosaidia pia kuiwezesha serikali kupunguza viwango vya kodi ya ongezeko la thamani siku za usoni kwa sababu walipakodi watakuwa wengi.
Kwa upande wake Balozi wa Uswizi aliyemaliza muda wake nchini Didier Chassot, ameipongeza Serikali kwa uamuzi huo wa kupitia mifumo ya kodi na kwamba anaamini mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao nchini watapata pia nafasi ya kuzungumza na kujadiliana na serikali kuhusu masuala hayo kama walivyoomba.
Balozi Chassot ametumia fursa hiyo ya kuagana na Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba kuipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa hatua kubwa iliyopiga kimaendeleo katika kipindi kifupi.
Ameahidi kuwa Uswisi inaandaa mpango mpya wa ushirikiano wa kimaendeleo na Tanzania, utakaojielekeza katika kufanikisha ajenda mbalimbali za maendeleo ya nchi kupitia programu zake mbalimbali ikiwamo kusaidia mfuko wa maendeleo ya jamii-TASAF, usimamizi wa fedha za umma, biashara na uwekezaji kupitia asasi za kiraia na sekta binafsi.
Didier Chassot ameitumikia nafasi hiyo ya ubalozi akiwa nchini kwa kipindi cha miaka minne na ameahidi kuendelea kuwa Balozi mzuri wa Tanzania atakaporejea nchini kwake kuendelea na majukumu yake mengine.