Latest Posts

DKT. NDUMBARO: WANANCHI MSIHADAIKE, UCHAGUZI NI HAKI YENU YA KIKATIBA

Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Damas Ndumbaro, ametoa wito kwa Watanzania wote kuwapuuza wanasiasa wanaowashawishi kutoshiriki katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, akisisitiza kuwa haki ya kushiriki uchaguzi ni ya kikatiba kwa kila Mtanzania mwenye vigezo.

Akizungumza Aprili 14, 2025 katika uzinduzi wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia katika uwanja wa Mashujaa, Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera, Dkt. Ndumbaro amesema kuwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iko wazi kuhusu sifa za kushiriki uchaguzi.

 

“Vigezo vya kumzuia mtu kushiriki uchaguzi ni kama si Mtanzania, ana matatizo ya akili, amehukumiwa kwa kosa la jinai, au hana kitambulisho cha mpigakura. Kama hauna kasoro hizo, kwanini usitumie haki yako?” alisisitiza Dkt. Ndumbaro.

Aidha, Waziri huyo amewakosoa baadhi ya wanasiasa wanaopotosha haki za binadamu kwa kuziangalia kisiasa pekee, huku wakisahau jitihada kubwa zinazofanywa na serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuboresha maisha ya wananchi kupitia ujenzi wa miundombinu na huduma za kijamii.

Katika mkutano huo, Dkt. Ndumbaro amewataka pia viongozi wa dini kukemea maovu, wakiwemo wale wanaojichukulia sheria mkononi, na kuwataka wananchi kujikita katika kutafuta suluhu ya migogoro badala ya kulimbikiza chuki, hasa migogoro ya ardhi na mirathi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fatma Mwassa, amesema serikali ya mkoa huo itachukua hatua kali kwa kuwafukuza kazi wenyeviti wa vijiji, mitaa na watendaji wanaochochea migogoro ya ardhi.

“Mkoa wa Kagera mara nyingi vifo na migogoro vinatokana na migogoro ya ardhi, inayosababishwa na baadhi ya viongozi wa vijiji kuuza maeneo kiholela. Sasa tumepanga kuwawajibisha wote wanaoendeleza migogoro,” amesema Mwassa.

Mwassa ameongeza kuwa baada ya kampeni hiyo ya msaada wa kisheria, mkoa umejipanga kuendeleza huduma hizo kwa wananchi kupitia uzoefu utakaopatikana kwenye utekelezaji wa kampeni hiyo ya Mama Samia katika halmashauri zote za mkoa huo.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!