Mgombea wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameahidi kuendelea kuimarisha sekta za kilimo na mifugo katika wilaya ya Geita kwa kujenga miundombinu ya kisasa itakayowezesha wafugaji na wakulima kunufaika zaidi na shughuli zao.
Akizungumza leo, Oktoba 12, 2025, katika mkutano wa kampeni uliofanyika Nyawilimilwa mkoani Geita, Dkt. Samia amesema katika kipindi cha miaka mitano iliyopita serikali imewekeza nguvu kubwa katika kuboresha sekta ya ufugaji, ikiwemo kutoa ruzuku za chanjo na kujenga miundombinu ya majosho na machinjio kwa ajili ya kulinda afya za mifugo na watumiaji wa bidhaa za nyama.
“Kwa upande wa ufugaji, katika miaka mitano tumewaona wafugaji kwa kuwapa ruzuku ya chanjo ili kuweka afya ya mifugo yetu. Tumetengeneza majosho, tumejenga mabwawa ya kunyweshea wanyama na machinjio yenye hali nzuri ili kuhakikisha afya ya watumiaji inalindwa,” amesema Dkt. Samia.
Ameongeza kuwa serikali yake itatekeleza ahadi ya kujenga machinjio mapya ya kisasa katika maeneo ya Nyawilimilwa na Nzera, pamoja na majosho 11 ndani ya wilaya ya Geita, hatua itakayosaidia kuboresha zaidi huduma za mifugo katika eneo hilo.
“Miongoni mwa ahadi zetu ni kujenga machinjio haya hapa Nyawilimilwa, kule Nzera na kwingineko. Tutajenga machinjio ya kisasa na majosho 11 ndani ya wilaya hii ya Geita,” amesema.
Aidha, akizungumzia sekta ya kilimo, Dkt. Samia amesema serikali itaimarisha mfumo wa vituo vya ukodishaji zana za kilimo, ikiwa ni sehemu ya mpango wa kuongeza tija na kuwapunguzia wakulima gharama za uzalishaji.
Dkt. Samia alibainisha kuwa mpango huo ni sehemu ya jitihada za serikali za kuwezesha wananchi kiuchumi kupitia kilimo cha kisasa na ufugaji wenye tija, akisisitiza kuwa sekta hizo ndizo uti wa mgongo wa uchumi wa Tanzania.