Mgombea wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameahidi kuendelea kuboresha huduma za afya katika wilaya ya Geita, ikiwemo kuongeza vifaa tiba vya kisasa na kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi.
Akizungumza leo, Oktoba 13, 2025, katika mkutano wa kampeni uliofanyika kata ya Nyawilimilwa wilayani Geita, Dkt. Samia amesema serikali imewekeza katika sekta ya afya kwa kujenga zahanati, vituo vya afya, na kuboresha hospitali za wilaya, lakini bado ipo dhamira ya kufanya zaidi.
“Mbali na kujenga zahanati na vituo vya afya, tumefanya maboresho ya miundombinu ya afya ikiwemo hospitali ya wilaya ya Geita. Tutaendelea kuiboresha hospitali hiyo na kuleta mashine za kisasa za vipimo, X-ray zinazotembea kitanda kwa kitanda, pamoja na CT-Scan kwa ajili ya uchunguzi wa kina wa afya za wananchi,” amesema Dkt. Samia.
Ameongeza kuwa serikali chini ya uongozi wake itahakikisha kila mwananchi anapata huduma bora za afya bila kulazimika kusafiri umbali mrefu, kwa kuongeza vituo vya afya na zahanati mpya katika maeneo ya pembezoni.
“Tutakapopata ridhaa tena, tutaongeza vituo vya afya na zahanati ili wale walioko mbali wasongezwe huduma kwa karibu,” amesisitiza.
Aidha, Dkt. Samia ameeleza kuwa serikali imepiga hatua katika maandalizi ya mpango wa bima ya afya kwa wote, ambao utazinduliwa kwa majaribio hivi karibuni, lengo likiwa kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma za afya kwa uhakika bila kikwazo cha gharama.
“Tutakapokuwa na bima ya afya kwa wote, masuala kama mtu kufariki na maiti kuzuiwa hospitalini kwa kushindwa kulipa gharama hayatakuwepo tena, kwa sababu bima ndiyo italipa gharama hizo,” amesema Dkt. Samia.
Amehitimisha kwa kusisitiza kuwa dhamira ya serikali ni kuhakikisha huduma za afya zinabaki kuwa za watu wote, bila ubaguzi, kwa kuzingatia falsafa ya “Kazi na Utu” inayolenga kumwinua kila Mtanzania.